IQNA

Papa Francis ajizuia kuwataja 'Waislamu wa Rohingya' akiwa Myanmar

13:18 - November 29, 2017
Habari ID: 3471287
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi wa Wakatoliki duniani Papa Francis amejizuia kuwataja Waisalmu wa Rohingya alipohutubu Jumanne akiwa Myanmar pamoja na kuwa jamii hiyo ya waliowachache inakabiliwa na mauaji pamoja na maangamizi ya kizazi nchini humo.

Akizungumza katika mji mkuu wa Myanmar, Naypyitaw, akiwa ameandamana na kiongozi wa kiraia wa nchi hiyo, Aung San Suu Kyi, Papa Francis ametosheka tu na kutoa wito wa umoja kuheshimuwa haki za Wamyanmar wote.

Safari ya Papa nchini Myanmar inakuja wakati ambao Waislamu Warohingya wapatao 620,000 wamelazimika kukimbia kutoka jimbo la Rakhine na kuelekea Bangladesh kutokana na kukandamizwa na kuuawa mikononi mwa jeshi la nchi hiyo na Mabuddha wenye misimamo mikali. Umoja wa Mataifa umetaja kile kinachowakumba Waislamu Warohingya kuwa ni maangamizi ya kimbari.

Kabla ya kuelekea Myanmar, Papa alishauriwa asiwatetee Waislamu wa Rohingya na wala asiwataja katika hotuba zake ili kuepusha mgogoro wa kidiplomasia ambao unaweza kutumiwa na jeshi pamoja na serikali ya dhidi ya Wakristo ambao pia ni jamii ya waliowachache nchini humo.

Papa Francis amekosolewa kwa kushindwa kutumia nafasi yake hiyo kulaani mauaji ya Waislamu akiwa safarini Myanmar.

Waislamu Warohingya wakiwa katika kambi ya Wakimbizi Bangladehs baada ya kukimbia jinai nchini Myanmar

Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani jinai na ukatili unaofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kusisitiza kuwa, huo ni mfano wa wazi wa kuangamiza kizazi na kaumu ya watu wa jamii fulani.

Jinai kubwa zaidi dhidi ya Waislamu wa Myanmar zimefanywa na jeshi la nchi hiyo na Mabudha wenye chuki za kidini katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo. Jinai hizo zimepamba moto tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu wa 2017 ambapo baadhi ya duru zinasema hadi sasa Waislamu zaidi ya 6,000 wameuawa.

3464551

captcha