IQNA

Misikiti 109 yafunguliwa upya Diyala, Iraq baada ya ISIS kutimuliwa

20:28 - February 24, 2018
Habari ID: 3471402
TEHRAN (IQNA)-Idara ya Waqfu wa Ahul Sunna katika mkoa wa Diyala nchini Iraq imesema misikiti 109 imefunguliwa tena baada ya kufunguwa kwa miaka mitatu kutokana na hujuma ya magaidi wa ISIS au Daesh katika eneo hilo.

Mkuu wa idara hiyo ya Waqfu Sheikh Taha Mujami amesema misikiti hiyo ilifungwa mwaka 2014 kwa sababu za kiusalama. Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kuwa usalama umerejea, sasa misikiti hiyo imefunguliwa tena ili kuendeleza shughuli za kawaida za ibada.

Mmoja kati ya misikiti iliyofunguliwa ni Masjid Mus'aib bin Umair karibu na mji wa Baqubah. Msikiti huo ulilengwa na magaidi wa ISIS ambao waliushambulia kwa mabomu na kupelekea watu kadhaa kuuawa na kujeruhiwa.

Mujami pia amepongeza nafasi chanya ya maafisa wa usalama katika kudumisha usalama katika maeneo ya ibada mkoani humo.

Magaidi wa ISIS, wakipata himaya ya madola ya kigeni na baadhi ya tawala za Kiarabu, waliteka maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq katikati ya mwaka 2014 baada ya kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa ya Syria. Magaidi hao wa ISIS walitangaza kile walichodai kuwa eti ni dola la Kiislamu au khilafa ambayo ilipata umaarufu kwa jinai na ukatili wake dhidi ya raia.

Lakini Disemba mwaka 2017, Jeshi la Iraq likishirikiana na wapiganaji wa kujitolea wa wananchi maarufu kama Hashd al-Shabi walifanikiwa kuwatimua kikamilifu magaidi hao wa Kiwahhabi wa ISIS kutoka maeneo yote walioyokuwa wameyateka nchini humo. Katika nchi jirani ya Syria halikadhalika magaidi wa ISIS wametiuliwa kutoka katika aghalabu ya ngome zao.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 wakati magaidi walipoivamia nchini hiyo kwa kimaya ya Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao wakiwemo Uingereza na Ufaransa kwa lengo la kubadilisha mlingano wa kieneo kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Kufuatia hujuma hiyo, Syria iliomba msaada wa Russia na Iran katika kuisaidia kukabiliana na magaidi.

3693941

captcha