IQNA

Misikiti Yote China Sharti Kupeperusha Bendera ya Taifa

18:51 - May 22, 2018
Habari ID: 3471527
TEHRAN (IQNA)- Misitiki yote nchini China imetakiwa kupeperusha bendera ya taifa hilo katika maeeneo ya juu na muhimu ya msikiti, Jumuiya ya Kiislamu China imetangaza.

Jumuiya hiyo, kupitia taarifa iliyochapishwa katika tovuti yake, imesema bendera hizo zitapeperushwa misikitini kwa lengo la kuimarisha moyo wa uzalendo miongoni mwa Waislamu. Hatua hiyo ambayo ni amri ya serikali inayotolewa kupitia Jumuiya ya Kiislamu China, imetathminiwa ni kati ya sera za chama tawala cha Kikomunisti kudhibiti dini na hasa kuzidi kuwabana Waislamu nchini humo.

Halikadhalika taarifa hiyo imetaka misikiti yote nchini humo kubandika matangazo ya Chama cha Kikomunisti kuhusu itikadi za ujamaa na kuzifafanua kwa kutumia aya za Qur'ani au Hadithi ili  'ziweze kukita mizizi katika nyoyo za watu.'

Jumuiya ya Kiislamu China ni taasisi inayofungamana na serikali na ndio taasisi pekee yenye uwezo wa kuwapa vibali Maimamu wa misikiti.

Amri hii mpya inakuja baada ya kupitishwa kanuni mpya za kidini mwezi Februari ambazo zilitaka misikiti kufunza katiba ya China pamoja na utamaduni wa  nchi hiyo.

Mwezi Januari pia mwaka huu Waislamu zaidi ya 100,000 kutoka jamii ya Uighur nchini China waliripotiwa  kushikiliwa kwa nguvu katika kambi zenye msongamano mkubwa ambapo wanafunzwa itikadi za Kikomunisti.

Kambi hizo, ambazo zinashabihiana na kambi za kulazimisha kufanya kazi za  laogai za zama za Mao, zinashikilia karibu Waislamu 120,000 katika eneo la Kahgar katika jimbo la Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.

Uislamu ni kati ya dini tano ambazo zinatambuliwa rasmi na Chama cha Kikomunisti China ambapo kuna takribani Waislamu milioni 23 nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeongezeka sera za kuwakandamiza Waislamu katika nchi hiyo hasa katika jimbo la  Xinjiang wenye Waislamu Zaidi ya milioni 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

3465909

captcha