IQNA

Waislamu China waandamana kupinga mpango wa kubomoa msikiti

6:07 - August 11, 2018
Habari ID: 3471625
TEHRAN (IQNA)- Maelfu ya Waislamu nchini China wamekusanyika katika msikiti mmoja kaskazini magharibi mwa nchi hiyo katika maandamano nadra ya kupinga mpango wa kuubomoa.

Kwa mujibu wa taarifa, siku ya Alhamisi Waislamu wa jamii ya Hui walikusanyika katika Msikiti wa Jamia wa Mji wa Weizhou ili kupinga mpango wa serikali ya kubomoa eneo hilo la ibada.

Msikiti huo unaolengwa kubomolewa ulimaliza kujengwa mwaka uliopita na hivyo Waislamu wameshangazwa na habari za mpango wa kuubomoa. Baadhi ya duru zinasema serikali inalenga kubomoa kuba nane kati ya tisa katika msikiti huo kwa madai kuwa jengo hilo ni kubwa zaidi ya ilivyoidhinishwa. Lakini Waislamu wa eneo hilo wamesema watapinga vikali mpango huo.

La kushangaza ni kuwa hata chama cha kikomunisti katika mji huo kilitume ujumbe wa pongezi wakati wa kuanza ujenzi wa msikiti huo lakini sasa inaonekana kuna mabadiliko katika msimamo wa awali wa kuruhusu ujenzi huo.

Maandamano hayo yamekuja huku serikali ya China ikizidisha ukandamizaji Waislamu na kuwalazimu watangaze utiifu wao kwa Chama cha Kikomunisti ambacho kimejengeka katika msingi wa kutomuamini Mwenyezi Mungu.

Katika Mikala ya hivi karibuni kuba za misikiti  zimebomolewa na nembo za nyota na hilali kuondolewa katika majengo ya misikiti.

Chini ya urais wa Xi Jinping, Chama cha Kikomunisti China kimeongeza ukandamizaji wa Waislamu kwa madai kuwa wana misimamo mikali.

Uislamu ni kati ya dini tano ambazo zinatambuliwa rasmi na Chama cha Kikomunisti China ambapo kuna takribani Waislamu milioni 23 nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeongezeka sera za kuwakandamiza Waislamu katika nchi hiyo hasa katika jimbo la  Xinjiang wenye Waislamu Zaidi ya milioni 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

3737317

captcha