IQNA

Mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Abu Dhabi

11:34 - November 02, 2021
Habari ID: 3474504
TEHRAN (IQNA)- Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu utafanyika Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mwezi Disemba.

Kongamano hilo ambalo limepewa anuani ya "Umoja wa Kiislamu, Fikra, Fursa na Changamoto' limeandaliwa na Baraza la Jamii za Waislamu Duniani.

Kwa mujibu wa taarifa, mkutano huo ambao unafanyika kwa himaya ya Waziri wa Masuala ya Stahamala UAE Sheikh Nahyan bin Mubarak Al Nahyan, utaanza Disemba 12 na kuendelea kwa siku tatu.

Akizungumza na waandishi habari Jumapili,  mwenyekiti wa Baraza la Jamii za Waislamu Duniani Ali Rashid al Nuaimi amesema kikao hicho kitajadili masuala ya kisheria na kielimu yanayohusu jamii za Kiislamu duniani kote. Aidha amesema kongamano hilo pia litajadili changamoto zinazowakabili Waislamu na kisha kutoa mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo.

Baraza la Jamii za Waislamu Duniani ni taasisi ya kimataifa isiyo ya kiserikali yenye makao yake katika mji wa Abu Dhabi. Baraza hilo linajumuisha taasisi 900 za Kiislamu kutoka nchi 142 kwa lengo moja ambalo ni kujumuishwa jamii za Waislamu katika nchi wanazoishi huku wakizingatia mafundisho sahihi ya Kiislamu.

4009847

captcha