Mkutano kati ya Mahmoud Farazandeh na Shiekh Ahmad El-Tayyib ulifanyika katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Sheikh El-Tayyib alionya kwamba hitilafu na migawanyiko iliyopo kati ya Waislamu inatokana na migogoro isiyo ya Kiislamu ambayo Qur'ani Tukufu ilitahadharisha juu yake. Amesema migogoro hiyo inapelekea kupotea kwa umoja wa Kiislamu, kugawanyika kwa jamii ya Kiislamu na kutokuwepo kwa dira ya pamoja baina ya Waislamu.
Ameongeza kuwa licha ya tofauti hizo, Waislamu bado wana malengo ya pamoja ya Kiislamu ambayo wanaweza kuyarejelea. Amesisitiza kuwa, changamoto ya dharura zaidi kwa Ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa ni kuwashawishi wanasiasa na wasimamizi wa maamuzi kwamba maslahi na thamani za Kiislamu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote. Alisema kwamba Waislamu wote lazima wakubaliane juu ya kanuni hii.
Aidha amesema wanazuoni wa Kiislamu wamesisitiza mara kwa mara umuhimu wa umoja wa Kiislamu, lakini mara nyingi madola ya kisiasa yanatenda kinyume na mantiki na malengo ya Uislamu.
Alipendekeza kuwa suluhu la mgogoro huu ni kupitisha mfumo wa kimaadili na wa kibinadamu ambao unatanguliza maslahi ya binadamu badala ya ubinafsi.
Balozi Farazandeh alielezea kufurahishwa kwake na kukutana na Sheikh El-Tayyib na akasifu juhudi zake za kuunganisha ulimwengu wa Kiislamu. Amesema Iran inatambua nafasi ya Kituo cha Kiislamu cha al-Azhar katika kuwaunganisha Waislamu na kuwaongoza kwenye njia sahihi dhidi ya wale wanaojaribu kupotosha sura ya Uislamu.
Pia alisema kuwa Iran imekubali mwaliko wa Sheikh El-Tayyib wa kushiriki katika mazungumzo ya Kiislamu wakati wa Mazungumzo ya IISS ya Manama mnamo Novemba 2023.
3485140