IQNA

Misikiti yafunguliwa tena Tripoli, Libya baada ya miezi saba

20:29 - October 10, 2020
Habari ID: 3473248
TEHRAN (IQNA) – Misikiti imefunguliwa tena katika mji mkuu wa Libya, Tripoli baada ya kufungwa kwa muda wa miezi saba ili kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Misikiti hiyo imefunguliwa kufuatia idhini iliyotolewa na Serikali ya Mafaka wa Kitaifa (GNU) huku nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni saba ikiwa imeripoti kesi 41,000 za corona na vifo 621 kutokana na ugonjwa hio hadi sasa.

Misikiti hiyo imefunguliwa mjini Tripoli na miji ya karibu kwa sharti la kuzingatia kanuni za kiafya ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa na kutokaribiana waumini wanaposwali. Aidha wanaoswali wametakiwa kubeba mkeka au zulia binafasi kwa ajili ya kuswali. Misikiti ambayo itakaidi kanuni hizo za afya itafungwa.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao makuu yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar ambaye ni kinara wa wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya, na nyingine ya Mwafaka wa Kitaifa, yenye makao yake Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

3472774/

captcha