IQNA

Jumuiya ya Wahadhiri wa Kiislamu Iran yalaani sera zilizo dhidi ya Uislamu Ufaransa

11:43 - October 11, 2020
Habari ID: 3473250
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Wahadhiri katika Chuo cha Kiislamu cha Qum, nchini Iran imelaani vikali pendekezo la serikali ya Ufaransa la kuweka vizingiti katika harakati za Kiislamu nchini humo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa hivi karibuni, ikiwa ni katika kuendeleza sera zake za chuki dhidi ya Uislamu, aliwasilisha muswada wa sheria dhidi ya Uislamu na kudai kuwa sheria hiyo inalenga kukabiliana na kile alichokitaja kuwa eti ni misimamo mikali.

Jumuiya ya Wahadhiri katika Chuo cha Kiislamu cha Qum imetoa taarifa leo na kusema: "Matamshi yaliyojaa chuki yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Ufaransa yamepotosha uhalisia wa mambo kuhusu dini tukufu ya Kiislamu na ni yenye kuibua chuki."

Aidha wasomi hao wa Kiislamu katika mji wa Qum nchini Iran wamelaani aina yoyote ya hatua dhidi ya dini na dhidi ya Uislamu huku wakitoa wito kwa jamii za Magharibi zirejee katika dini na umaanawi.

Taarifa hiyo imesema Uislamu unaopigiwa debe na Marekani ni ule ambao umeibuliwa katika vituo vya utafiti vya Wazayuni kwa msaada wa kifedha wa nchi za Magharibi. Taarifa hiyo imesema Uislamu huo potovu ndio unaopigiwa debe katika vyombo vya habari vya Magharibi na ndio chanzo cha misimamo mikali ya kidini katika nchi za Ulaya.

Jumuiya ya Wahadhiri katika Chuo cha Kiislamu cha Qum imesema Ufaransa itafeli katika njama zake hizo dhidi ya Uislamu na kwamba vijana wenye kutafuta ukweli wataweza kuusoma na kuujua Uislamu halisi. Hali kadhalika taarifa hiyo imesema undumakuwili wa nchi za Magharibi katika kukabiliana na ugaidi ndio chanzo cha matatizo yaliyomo. Aidha taarifa hiyo imehoji ni vipi Ufaransa inadai kupambana na misimamo mikali wakati imelewa kwa dola za mafuta na inafungamana na wanaoeneza ukufurushaji, uwahhabi na ugaidi ambao ni chanzo cha kumwagika damu katika nchi za Kiislamu kama vile Yemen na Iraq?

Taarifa hiyo pia imetoa wito kwa wasomi kote duniani kutafakari kuhusu njia za kuwepo maingiliano mema baina ya wafuasi wa dini za mbinguni.

84070780/

captcha