IQNA

Mateka Wapalestina wasusia chakula katika jela za Israel kumuunga mkono wenzao

11:02 - October 12, 2020
Habari ID: 3473252
TEHRAN (IQNA)- Hali ngumu na isiyo ya kibinadamu ya magereza ya utawala wa Israel imepelekea mateka au wafungwa kadhaa kususia chakula kama njia ya kubainisha malalamiko yao.

Maher al-Akhras na Wael al-Jaghoub ni mateka wawili Wapalestina ambao kwa muda sasa wamesusia kula chakula na sasa taasisi za Kiapelestina zinasema hali yao ni mbaya mno.

Kwa kuzingatia hali hiyo, mateka 30 wa Kipalestina katika gereza ya Ofer, ambao ni wanachama wa Harakati ya Jihad Islami, Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, wameamua kususia chakula katika kuwaunga mkono Maher al Akhras na Wael al-Jaghoub,

Karibu mateka 4,800 wa Palestina wakiwemo wanawake 41 na watoto 140 wanashikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel. Mateka hao wa Palestina ni kati ya waathirika wakubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa Abdul–Nasser Farwana, mkuu wa kitengo cha utafiti na ukusanyaji nyaraka katika Kamati ya Masuala ya Wafungwa wa Palestina, tokea mwaka 1967, Wapalestina 222 wamekufa shahidi katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Anasema mateka 75 wamekufa shahidi kutokana na njama za moja kwa moja makusudi za utawala wa Kizayuni  huku saba wakipoteza maisha kutokana na majeraha waliyopata baada ya kupigwa risasi na  wanajeshi wa utawala wa Kizayuni ambapo walikufa shahidi baada ya kuhamishiwa gerezani. Wafungwa wengine 67 wa Palestina wamekufa shahidi katika jela za Israel kutokana na kunyimwa dawa baada ya kuugua huku wengine 73 wakifa shahidi kutokana na mateso makali waliyopata gerezani.

Kwa msingi huo tokea zamani mateka Wapalestina wamekuwa wakiishi katika hali mbaya sana katika gereza za utawala wa Israel na sasa baada ya kuibuka janga la corona hali yao imezidi kuwa mbaya.

Utawala wa Israel umekataa kuwapa mateka Wapalestina huduma na suhula la afya. Moja ya hatua zilizo dhidi ya binadamu ambazo Israel imechukua dhidi ya mateka Wapalestina ni kuwatuma madaktari walioambukizwa corona kuhudumu katika gereza hizo. Mbali na hayo, wafungwa Wapalestina wananyimwa ruhusa ya kuwasiliana na familia zao jambo ambalo limepelekea familia hizo ziingiwe na wasi wasi mkubwa. Hali ngumu na isiyo ya kibinadamu ya magereza ya Israel imepelekea mateka kadhaa kususia chakula kama njia ya kubainisha malalamiko yao.

3928558

captcha