IQNA

Marekani yatakiwa iiwajibishe Saudia kuhusu mauaji ya Khashoggi

22:19 - October 02, 2021
Habari ID: 3474373
TEHRAN (IQNA) - Mke wa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyeuawa kinyama mikononi mwa maajenti wa Ufalme wa Saudi Arabia huko Uturuki ameitaka Marekani iuwajibishe ufalme huo kutokana na mauaji ya kinyama ya mwandishi na mkosoaji huyo.

Khadija Genghis ametoa ombi hilo miaka mitatu baada ya mauaji hayo ya kutisha yalifofanywa kwa amri ya mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman. 

Genghis yuko mjini Washington kwa ajili ya kushiriki katika maandamano yanayofanyika mbele ya ubalozi wa Saudia katika kumbukumbu ya mwaka wa 3 tangu Jamal Khashoggi auawe mjini Istanbul.

Mjane huyo  ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan ya kukutana na kufanya mazungumzo na mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman  ambaye taasisi za upepelezi zinasema ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa mwandishi na mkosoaji huyo wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia. Mazungumzo hayo yanafanyika sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa tatu tangu Khashoggi alipouliwa.

Itakumbukwa kuwa, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia wa gazeti la Washington Post aliuawa kinyama mwaka 2018 kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme.

Khashoggi aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na mwili wake ukakatwa vipande vipande.  

3475878

captcha