IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Uwepo wa askari vamizi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi ni chanzo cha mfarakano

21:23 - October 03, 2021
Habari ID: 3474375
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uingiliaji na uwepo wa askari vamizi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ni chanzo cha mfarakano na uharibifu katika kanda hii.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili mjini Tehran wakati alipohutubu kwa njia ya video katika mahafali ya pamoja ya makadeti waliohitimu Vyuo vya Kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Imam Hussein AS.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran, amesema majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sawa na ukuta madhubuti na ngao imara ya kuzima vitisho vya maadui wa ndani na nje ya taifa hili.

Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa, "Hii leo, vikosi vya majeshi ya Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), jeshi la polisi, pamoja na vikosi vya kujitolea (Basiji) ni ukuta madhubuti mkabala wa vitisho vya maadui." 

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, masuala ya eneo hili yanapaswa kupatiwa ufumbuzi pasi na kuzishirikisha nchi ajinabi. Ameeleza kuwa, nchi za eneo hili zinapaswa kuiga mfano wa Iran wa kutumia mantiki licha ya kuwa ni taifa lenye nguvu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema matukio yanayoshuhudiwa katika eneo hili la Magharibi mwa Asia, kaskazini magharibi mwa Iran na kwengineko yanapaswa kufumbuliwa kwa kutumia mantiki hiyo hiyo ya kutoyashirikisha mataifa ajinabi.

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, majeshi ya eneo hili yana uwezo wa kulinda usalama na kwamba nchi za kanda hii hazipaswi kuruhusu uingiliaji au uwepo wa majeshi ajinabi.

Amesema katika hali ambayo usalama ni kitu cha kawaida katika taifa la Iran, lakini baadhi ya nchi zikiwemo za Ulaya zimeshindwa kujidhaminia usalama.   

4001948

captcha