IQNA

Chanjo ya COVID-19 yatolewa karibu na msikiti Abuja, Nigeria

11:29 - October 10, 2021
Habari ID: 3474406
TEHRAN (IQNA)-Waislamu katika mji wa Abuja, Nigeria wamepokea chanjo ya COVID-19 nje ya msikiti baada ya Sala ya Ijumaa.

Shughuli hiyo imefanyika nje ya Msikiti wa Kuje mjini Abuja, ambapo Imamu amepokea chanjo ya COVID-19 kama njia ya kuwahimiza waumini nao pia wadungwa chanjo hiyo.

Hadi sasa watu wa Nigeria wamedungwa dozi milioni saba za chanjo ya COVID-19 katika nchi ambayo ina jumla ya watu milioni 206.

Mmoja wa viongozi wa msikiti huo Alhaji Lubisalah amekaribisha jitihada hizo za serikali za kukabiliana na COVID-19 lakini amewataka wakuu wa nchi kushughulikia zaidi ugonjwa wa Malaria ambao unaua watu kuliko COVID-19.

Wiki iliyopita, Shirika la Afya duniani WHO limeidhinisha chanjo ya kwanza ya ugonjwa wa Malaria likisema inapaswa kutolewa kwa watoto kote afrika, kwa matumaini kwamba itachochea jitihada zilizokwama za kuzuia kuenea kwa maradhi hayo. 

WHO imesema uamuzi wake umetokana na matokeo ya utafiti unaoendelea katika nchi za Ghana, Kenya na Malawi ambao uliwafuatilia watoto zaidi ya 800,000 waliopatiwa chanjo ya Malaria tangu mwaka 2019.

Kiasi cha dozi milioni 2.3 za chanjo hiyo zilitolewa kwa watoto wadogo katika nchi hizo tatu. Programu hiyo ilifuatiwa na majaribio kadhaa ya kliniki katika nchi saba za Afrika.

Malaria ni ugonjwa unaotajwa kuwa mbaya zaidi kuliko COVID-19 barani Afrika. Kulingana na takwimu za WHO, ugonjwa huo uliua Waafrika wapatao 386,000 mnamo 2019, ikilinganishwa na vifo 212,000 vya COVID-19 katika kipindi cha miezi 18.

Shirika hilo la afya ulimwenguni linasema asilimia 94 ya visa na vifo vya malaria vinatokea Afrika, bara lenye watu bilioni 1.3. 

3475967

Kishikizo: nigeria abuja msikiti COVID
captcha