IQNA

Wasifu mfupi wa Sheikh Hassan Mwalupa

12:10 - October 10, 2021
Habari ID: 3474408
Mnamo 14 Dhul Hija 1442 Hijria Qamaria sawa na 25 Julai 2021, Waislamu wa Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani walikumbwa na majonzi kufuatia kuaga dunia mwanazuoni mtajika wa Kiislamu na mfasiri wa Qur’ani Tukufu Alhaj Sheikh Hassan Mwalupa.

Alipoteza maisha akiwa anapata matibabu mjini Mombasa na kuzikwa katika eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale mnamo 15 Dhul Hija 1442 Hijria Qamaria.

Kifo cha  Shekh Mwalupa kilikuwa ni pigo kubwa si tu kwa familia yake, wanafunzi na wanazuoni wenzake, bali pia kwa jamii nzima ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Afrika Mashariki.

Mzawa wa Tanga

Sheikh Mwalupa alizaliwa Tanga, Tanzania mnamo Novemba 8 1957 na katika utotoni alijiunga na Madrasatu Shamsiyya na mjini hapo kujifunza lugha ya Kiarabu. Baadaye alielekea Mombasa, Kenya na kujiunga na taasisi ya Bilal Muslim Mission kwa lengo la kuendeleza masomo yake chini ya Maulana Sheikh Zaffar Abbas (ambaye sasa yuko Uingereza). Baada ya kumaliza masomo yake alifanya kazi kama Maalim katika eneo la Mackinnon Road katika kaunti ya Kwale kabla ya kurejea Tanzania.

Masomo Iran

Akiwa nchini Tanzania, alipata fursa ya kuendeleza masomo mjini Tehran katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Akiwa masomoni hapo alipata kufahamiana na wasomi waliobobea katika vyuo vya kidini au Hawza wakiwemo mandugu wawili Ayatullah Haadi Mudarisi na Ayatullah Taqi Mudarisi.

Baada ya kumaliza masomo alirejea Mombasa na hapo akaanza kazi ya tarjuma ya vitabu vya Kiarabu kwa lugha ya Kiswahili. Kati ya vitabu ambavyo alivutarjumu wakati huo ni Tafsiri ya Al Mizan ya Allamah Tabatabai ambapo alifanikiwa kukamilisha Juzuu ya 30 yaani Juzu Amma. Kabla  hajaaga dunia alikuwa anatayarisha chapa ya pili ya Juzu Amma ya Tafsir al Mizan.

Madrastu Amir ul Muimineen

Alifanikuwa kuanzisha chuo  cha Madrastu Amir ul Muimineen akishirikiana na Sheikh Abdillahi Nassri huko Matuga. Chuo hicho kimeweza kupata mafanikio makubwa ambapo hadi sasa wanafunzi 35 wa chuo hicho wameweza kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kuendeleza masomo yao ya Kiislamu. Idadi kubwa ya wanafunzi hao wameweza kujiendelea vizuri kielimu na sasa wanauhudumia Umma kama Maimamu misikitini, waalimu wa Madrassah n.k. katika vituo mbali mbali vya Kiislamu Afrika Mashariki. Kwa ujumla wanafunzi takribani 3000 wamesoma moja kwa moja chini ya Marhum Alhaj Sheikh Hassan Mwalupa na daima watamkumbuka kama kigezo bora cha kuigwa.     

Miradi

Sheikh Mwalupa aliandaa warsha na kozi mbali mbali kwa waalimu kutoka taasisi mbali mbali ili kuwawezesha wajiboresha kitaaluma. Hadi wakati wa kifo chake, alikuwa akirekodi vipindi katika Televisheni ya IBN TV Africa na pia alikuwa akisomesha kwa njia ya intaneti katika Bilal Muslim Mission ya Kenya.

Alikuwa akishirikiana na Taasisi ya Al Itrah ya Dar es Salaam Tanzania katika miradi ya tarjuma na kila mwezi alikuwa katika mji huo kwa muda wa siku 10 kuhakikisha miradi husika inakamikila.

Miradi yake muhimu zaidi katika Al Itrah ilikuwa ni pamoja na:

  • Kutarjumi kwa Kiswahili juzuu saba za Tafsiri ya Qur’ani ya Al Kashif ya Allama Mohammad Jawad Mugnyiyya
  • Tarjuma ya Qur’ani Tukufu ya Kiarabu kwa lugha ya Kiswahili
  • Mradi uliokuwa ukiendelea wa tafsiri yake ya Qur’ani Tukufu ambayo imekamilika na sasa kilichobakia ni kuihariri.
  • Aidha alikuwa na mradi ambao ulikuwa bado haujakamilika wa kuihariri Tafsir al Kashif ya Kiswahili ambayo ilikuwa na juzuu 30 na kuifupisha kuwa na juzuu sita.

Tarjuma ya Kiswahili ya Al Kashif ya Allama Jawad Mughniya ambayo Marhum Sheikh Mwalupa ameitarjumu kwa Kiswahili imetajwa na weledi wengi kuwa kazi bora ya aina yake. Leo Maimamu wengi katika Sala za Ijumaa huinukulu tarjumu hii mara kwa mara. Alhamdulillah alikuwa na ujasiri wa kuandika Tafsiri yake ya Qur’ani Tukufu ambayo sasa inaharirriwa kabla ya kuchapishwa hivi karibuni Inshallah. Mbali na kazi zake hizo pia aliweza kuhariri vitabu vingi vya Kiswahili ambavyo vimechapishwa.

Mwendazake alikuwa mwanazuoni mnyenyekevu, mwenye jitihada, muaminifu na mwenye nidhamu ya hali ya juu na alikuwa na nafasi muhimu sana katika kutangaza Uislamu na hasa madhehebu ya Ahul Bayt AS.

Kwa hakika kifo cha Sheikh Mwalupa kimeacha pengo kubwa ambalo itakuwa ni vigumu kulijaza. Tunamuomba Mwenyezi Mungu SWT amrehemu na aipe familia yake subira na ni matumaini yetu kuwa kazi alizoanzisha zitakamilishwa kwa mafanikio.

589587

captcha