IQNA

Darul Iftaa ya Misri yataka Waislamu waadhimishe Maulid ya Mtume Muhammad SAW

17:03 - October 12, 2021
Habari ID: 3474415
TEHRAN (IQNA) – Taasisi ya Darul Iftaa ya Misri imetoa wito kwa Waislamu dunaini kote kuandaa sherehe za kukumbuka kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW ambazo ni maarufu kama Maulidi.

Aidha Darul Iftaa imetaka Sunna hii ya Mtume SAW ihuishwe pasina kuzingatia matamshi ya wanaoiharamisha.

Katika taarifa ambayo imechapishwa katika tovuti ya El Balad, Darul Iftaa al Misriyyah, ambayo ni moja ya taasisi muhimu zaidi za kutoa Fatwa za Kiislamu duniani, imeandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa:"Kuna dalili chungu nzima ambazo zinaonyesha kuwa, Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW walisherehekea Maulid ya mtukufu huyo na yeye pia aliidhinisha kitendo hicho."

Darul Iftaa ya Misri imeongeza kuwa: "Mtume SAW binafsi pia alikuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Imenukuliwa kutoka kwa Muslim kutoka wa Abu Qatada RA kuwa, Mtume SAW alikuwa anafunga saumu siku ya Jumatatu na alikuwa akisema: 'Mimi nilizaliwa katika siku kama hii.' Kwa msingi huo kitendo hicho kilikuwa ni cha kushukuru kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa. Sisi pia tunapaswa kushukuru wakati wa Maulid ya Mtume wa Rahma SAW.

Aidha taasisi hiyo adhimu ya Fiqhi nchini Misri imesisitiza kuwa: "Maulamaa wa zamani na wa sasa kuanzia karne ya 4 Hijria hadi sasa wameafikiana kuwa inafaa kuandaa sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad SAW kiasi kwamba baadhi ya maulamaa na mafuqahaa wanasema kitendo hiki ni Mustahabu na wametoa dalili sahihu kuhusua na hili. Kwa msingi huyo, mtu mwenye ufahamu na akili salama hana dalili au sababu za kukana kile ambacho kilikuwa kikifanywa na maualmaa waliotangulia. Hii ni kwa sababu (hao maulamaa waliotangulia) walikuwa wakiandaa sherehe usiku wa Maulid ya Mtume SAW ambapo waliwalisha hadhirina na kulikuwa na vikao vya tilawa ya Qur'ani Tukufu, mbali na kusoma dhikri, dua na mashairi ya kumsifu Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW. Wanahistoria wengi kama vile Ibn Jawzi, Ibn Kathir na Ibn Dahiya al- Andalusi, Ibn Hajr na Jalaludin Suyuti wamethibitisha kuwepo sherehe kama hizo.

Sherehe za kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad SAW au Miladun Nabii ni kati ya Idi kubwa za Kiislamu ambapo Ahul Sunna wal Jamaa huamini siku hiyo ni 12 Mfungo Sita Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanaitakidi kuwa siku hiyo ni 17 Mfungo Sita Rabiul Awwal. Kipindi baina ya siku hizi mbili kimetangazwa nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni wiki ya kudhimisha Umoja wa Waislamu.

4003961

captcha