IQNA

Jeshi la Nigeria lathibitisha kuangamizwa kinara wa ISIS nchini humo

19:21 - October 15, 2021
Habari ID: 3474427
TEHRAN (IQNA)- Jeshi la Nigeria limethibitisha habari ya kuangamizwa kinara wa genge la kigaidi la Daeshi au ISIS kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi la Nigeria iliyotolewa jana ikisema kuwa, Abu Musab al Barnawi, mkuu wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko magharibi mwa Afrika ameuliwa na jeshi la Nigeria.

Hata hivyo hakukutolewa maelezo zaidi kuhusu namna mkuu huyo wa genge la kigaidi la Daesh Afrika Magharibi alivyouawa.

Ripoti zinasema kuwa, Abu Musab al Barnawi ambaye jina lake la asili ni Habib Yusuf alikuwa mwanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram kabla ya kujitenga na kuwa kiongozi wa genge la Daesh huko Nigeria.

Nigeria imekumbwa na mashambulio mengi ya kigaidi, ya kikatili na ya umwagaji wa damu katika miaka ya hivi karibuni. Mashambulizi hayo yalianzia kaskazini mwa nchi hiyo na baadaye kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo na hadi katika nchi jirani zinazopakana na Nigeria ambazo ni Niger, Chad na Cameroon.

Genge la Boko Haram lilijitokeza mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria kwa madai ya kupambana na kile kilichotajwa na genge hilo kuwa ni elimu za Magharibi. Kwa mujibu wa itikadi potofu za genge hilo la ukufurishaji, elimu zote linazodai ni za Magharibi, ni haramu na ndio maana ya neno Boko Haram.

Mwaka 2016 genge la Daesh (ISIS) lilijiengua kutoka kwenye genge la Boko Haram na kuanzisha genge jipya la kigaidi  lililolipachika jina la ISIS au Daesh Magharibi mwa Afrika (ISWAP).

Mwezi Septemba pia Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alidai kuwa jeshi la nchi yake limemuangamiza Adnan Abou Walid al-Sahrawi, kinara wa tawi kundi la kigaidi la ISWAP.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni walisisitiza kuwa, Afrika katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 imedhurika na kujipenyeza pakubwa makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida.

Wamesema, kujipenyeza pakubwa makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama Mali, Burkina Faso, Kodivaa, Niger, Senegal, Nigeria, Cameroon, Somalia, Kenya, Msumbiji na Tanzania ni jambo lenye kutia wasiwasi. 

Makundi ya magaidi wakufurishaji barani Afrika kama vile ISWAP, Boko Haram na Al Shabab, ambao wamewasababishia watu wa bara hilo hasara kubwa, hufuata itikadi kali ya Uwahhabi ambayo ni itikadi rasmi nchini Saudi Arabia.

/3476050

captcha