IQNA

Hujuma dhidi ya Msikiti wa Kishia Afghanistan yalaaniwa na Al Azhar, Mufti wa Misri

20:35 - October 16, 2021
Habari ID: 3474430
TEHRAN (IQNA)- Hujuma dhidi ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wakati wa Sala ya Ijumaa huko Kandahar, Afghanistan imelaaniwa vikali na Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar na Mufti wa Misri.

Kwa mujibu wa tovuti ya Masrawy, Al Azhar imesema kuibua mifarakano ya kimadhehebu na kutumia fursa hiyo kuua na kuwatisha raia wasio na hatia ni kitendo cha usaliti kwa mafundisho ya Kiislamu.

Al Azhar pia imesema wale wanaoua waumini katika nyumba ya Allah wameuza nafsi zao kwa thamani ya chini kabisa na bila shaka wataadhibiwa siku ya qiyama. Halikadhalika Al Azhar imesema wanaoibua fitina wanatumia vibaya tafauti zilizopo baina ya madhehebu za Kiislamu kuibua mifarakano lakini wanasahau kuwa Waislamu wa madhehebu zote wamekuwa wakiishi kwa amani kwa karne 14.

Kwa upande wake Mufti wa Misri Sheikh Shawki Allam amelaani hujuma hiyo ya kigaidi na kuitaja kuwa dhambi kubwa katika Uislamu na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu  kuua Mwislamu ni kitendo kibaya zaidi ya kuubomoa Msikiti Mtakatifu wa Makka.

Amesema watu wenye misimamo ya kufurutu adha hawaheshimu damu ya watu wasio na hatia wala maeneo ya ibada na kuongeza kuwa, vitendo kama hivyo ya kuhujumu misikiti vitawaweka mbali watu na Misikiti, Halikadhalika amewatahadharisha watu wenye misimamo mikali wanaifasiri vibaya  aya ya 33 ya Sura Al Ma’idah isemayo,  “Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa.”

Makumi ya watu waliokuwa katika Swala ya Ijumaa wameuawa shahidi na wengine karibu ya mia moja wamejeruhiwa katika milipuko miwili iliyotokea jana Ijumaa katika Msikiti wa Bibi Fatima katika mji wa Qandahar Afghanistan. Mamia ya watu waliuawa na kujeruhuhiwa pia katika mlipuko Ijumaa iliyopita walipokuwa katika Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Washia huko Kunduz Afghanistan.

Msikiti wa Washia kukumbwa na milipuko huko Afghanistan katika muda wa wiki moja. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limekiri kuhusika na hujuma hizo mbili za kigaidi dhidi ya misikiti wa Mashia wakati wa Sala ya Ijumaa.

Mlipuko wa jana Ijumaa umetokea katika hali ambayo kundi la Taliban ndilo linaloongoza huko Afghanistan; na baada ya mlipuko wa Kunduz liliahidi kuwa jinai kama hiyo haingekaririwa tena nchini humo na kwamba lina uwezo wa kuwadhaminia usalama wananchi wa Afghanistan khususan Waislamu wa Kishia. Taliban hivi sasa inakabiliwa na changamoto ya mashambulizi katika hali ambayo kundi hilo pia lilikuwa likitekeleza mashambulizi kama hayo katika utawala  wa zamani nchini humo; na sasa kundi linaloipinga Taliban kwa jina la Daesh linaendesha harakati na hujuma dhidi ya kundi hilo na wananchi wa Afghanistan. Hii ina maana kuwa, kundi la Taliban linajua vyema namna mashambulizi hayo yanavyotekelezwa na linaweza kuyadhibiti mara moja. Kwa msingi huo kukaririwa mashambulizi  ya kigaidi kama hayo katika Msikiti wa Washia ni jambo lenye kutia shaka. 

4005245

 

captcha