IQNA

Iran na Eneo

Iran yajibu kauli ya mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

19:34 - September 09, 2022
Habari ID: 3475754
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vipengee vya taarifa ya kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Nasser Kanani, ametoa jibu kwa vipengee vya taarifa ya kikao cha 158 cha  mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya ile inayojiita kamati ya pande nne kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: kutolewa taarifa kama hizo ni ishara ya kukosa ufahamu sahihi baadhi ya nchi zilizotajwa, kuhusiana na mwenendo wa matukio yanayojiri katika eneo na kujifanya hazijui ukweli halisi wa hali ya eneo la Asia Magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Kanaani ameongeza kuwa: badala ya nchi hizo kurudia tuhuma za kila mara na zisizo na maana, zijikite kushughulikia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Msemaji wa mambo ya nje wa Iran amebainisha pia kuwa, kutolewa taarifa kama hizo sambamba na hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi za kuboresha uhusiano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunaonyesha mgongano; na kwa mara nyingine tena akasisitizia msimamo wa kila mara wa Iran wa kuwaalika majirani zake kwa mazungumzo na kutatua sutafahamu zilizopo kupitia njia za kidiplomasia.

Kanani ametupilia mbali pia madai ya taarifa hiyo kuhusu visiwa vitatu vya Iran na akasema, hatua zote inazochukua Iran zinalenga kulinda mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya nchi na akalaani uingiliaji wa wengine katika suala hilo.
Aidha, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ameashiria uwezo wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kulinda usalama wa vyombo vya majini katika eneo la Ghuba ya Uajemi na jinsi vikosi hivyo vilivvyo macho na makini kukabiliana na chokochoko na hatua yoyote ya kuvuruga usalama wa baharini; na akatilia mkazo umuhimu wa usalama wa eneo kudhaminiwa na nchi zenyewe za kanda hii bila kuingiliwa na madola ya kigeni.
4084251
captcha