IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Waislamu huko Edmonton, Kanada wahudhuria mkutano kuhusu chuki dhidi ya Uislamu

16:18 - September 10, 2022
Habari ID: 3475762
TEHRAN (IQNA) – Waislamu katika eneo la Edmonton nchini Kanada (Canada) wametoa ushuhuda wenye nguvu kwa maseneta wa Baraza la Seneti la Kanada kuhusu uzoefu wao na ubaguzi wa rangi na uhalifu unaochochewa na chuki katika mkutano wa hadhara mjini humo.

Ni sehemu ya utafiti kote Kanada kuhusu chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) uliofanywa na Kamati ya Seneti ya Haki za Kibinadamu - uliopendekezwa na Seneta Salma Ataullahjan.

"Nilikuwa nikiangalia takwimu na nikagundua Waislamu wengi waliouawa katika nchi ya G7 walikuwa Canada - nilishtuka," Ataullahjan alisema Alhamisi.

Mwanachama wa kamati na seneta wa kwanza Muislamu, Mobina Jaffer, alisema wanataka kuifanya jamii ihisi kama wanasikilizwa.

"Unapokuja katika jiji na kusikia kutoka kwa watu namna wanavyokabiliana na chuki dhidi ya Uislamu, inanifanya nifikiri hii sio nchi ninayoijua - hii sio nchi niliyokuja," Jaffer alielezea. Ni suala linaloongezeka huko Edmonton.

Mapema mwaka huu, polisi waliwashtaki watu wanne kuhusiana na mashambulizi sita katika muda wa miezi kadhaa - yote yanaaminika kuchochewa na chuki.

Mnamo 2020, Edmonton ilirekodi vitendo 79 vya uhalifu wa chuki 79. Mnamo 2021, idadi hiyo iliruka hadi 116.

Jibril Ibrahim, rais wa Jumuiya ya Utamaduni ya Somali-Kanada ya Edmonton, alizungumza katika kikao hicho - mmoja wa mashahidi wengi akitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuhusu suala hilo.

"Isipokuwa kuna matokeo ya vitendo hivi, basi tutaona zaidi na zaidi," Ibrahim alisema.

"Jambo muhimu zaidi ambalo serikali ya shirikisho inapaswa kufanya ni kuangalia ufafanuzi wa uhalifu wa chuki."

Ibrahim alisema uhalifu huo kwa kiasi kikubwa hauripotiwi kwa sababu ya mwingiliano mbaya wa kihistoria na polisi, ikiwa ni pamoja na kutochukuliwa kwa uzito.

Huduma ya Polisi ya Edmonton ilisema inachukua uhalifu huu kwa uzito na wachunguzi wake wa uhalifu wa chuki wanataka kujua kuhusu matukio ya chuki.

"Chuki huathiri kila mtu na ina athari kubwa kwa waathiriwa na jamii nzima," msemaji wa EPS alisema katika taarifa.

"Kwa sababu hii, tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na washirika wetu wa jamii ili kujenga imani na kuhimiza raia kujisikia salama kutoa taarifa za uhalifu na matukio haya kwa polisi."

Maseneta walisema ni wazi kuna mambo mengi ya utafiti huo yachunguzwe kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kubadilisha neno Islamophobia.

"Ninafikiria tena jina hili lote sasa - Islamophobia," Ataullahjan alisema.

"Tumekuwa na wasemaji wakielezea wasiwasi - kuwa na woga inamaanisha kuwa unamuogopa mtu, lakini haishughulikii maswala ya Waislamu."

Kisha, kamati itaelekea Quebec na kisha kwenda Toronto. Utafiti huo umepangwa kuendelea hadi Novemba.

Matokeo kutoka kwa utafiti yataingia katika ripoti ambayo itatoa mapendekezo kwa serikali ya Kanada.

captcha