IQNA

Matembezi ya Arabeen

Wafanyaziara wa Siku ya Arbaeen katika Haram ya Imam Hussein AS

KARBALA (IRAQ)- Mamia ya maelefu ya wafanyaziara wamekuwa wakitembelea Haram ya Imam Hussein AS kila siku tokea mwanzo wa Mwezi wa Safar kwa mnasaba wa Arbaeen ya Imamu huyo mtoharifu.

Taarifa zinasema wafanyaziara milioni 20 wamekusanyika katika mji wa Karbala wa Iraq kuadhimisha Arbaeen, tukio la kila mwaka ambalo linaadhimisha siku ya 40 baada ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia.

Mjumuiko wa Arbaeen  huko Karbala Iraq, umetajwa kuwa mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini ulimwenguni, unaowaleta pamoja wa mamilioni ya wafanyaziara kutoka Iraq na Iran na pia kutoka mataifa mengine duniani..

Wafanyaziara  ambao aghalabu walivalia mavazi meusi kama ishara ya maombolezo walikusanyika katika haram tukufu ya Imam Hussein AS huko Karbala siku ya Jumamosi katika kilele cha matembezi ya zaidi ya wikki moja ya ukumbusho wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mohammad (SAW), ambaye aliuawa shahidi pamoja na masahaba zake wakati wa vita vya Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria au 680 Miladia.

Wanaume, wanawake, vijana na wazee walikusanyika kwa mamilioni katika mji huo wa Iraq ili kutoa heshima kwa Imam Hussein (AS), ambaye ni kiongozi na mbeba bendera ya vita dhidi ya dhulma na ukandamizaji.

Tukio hilo la kila mwaka, ambalo ni moja ya makusanyiko makubwa ya kidini duniani, huleta pamoja umati wa wapenzi na waumini wa Imam Hussein AS kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya matembezi ya kilomita 80 kati ya miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.