IQNA

Jinai za Israel

OCHA: Wapalestina milioni mbili Gaza wanateseka kutokana na mzingiro haramu wa Israel

17:45 - January 31, 2023
Habari ID: 3476492
TEHRAN (IQNA)- Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema zaidi ya Wapalestina milioni mbili huko Gaza (Ghaza) wanateseka kutokana na mzingiro wa miaka 16 wa utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo hilo.

OCHA ilisema katika ripoti mpya kwamba "vizuizi vya muda mrefu vya watu na bidhaa kutoka Gaza vimedhoofisha hali ya maisha ya zaidi ya wakazi milioni mbili wa Palestina."

"Israel inaendelea kupunguza upatikanaji wa riziki, huduma muhimu, na makazi, kuvuruga maisha ya familia, na kudhoofisha matumaini ya watu ya mustakabali salama na ustawi," imesema ripoti hiyo ya OCHA ambayo  imeongeza kuwa hali hii mbaya pia imechangiwa na vizuizi vilivyowekwa na mamlaka ya Misri huko Rafah.

Tangu mwaka 2007, utawala katili wa Israel uliweka mzingiro wake kinyume cha sheria kwenye Ukanda wa Gaza, wenye makazi ya zaidi ya watu milioni 2.3, baada ya harakati ya Kiislamu ya Hamas kushinda katika uchaguzi huru wa wabunge mwaka 2006.

Aidha utawala haramu wa Israel umeanzisha vita vikubwa vitano vya kijeshi dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kuua na kujeruhi maelfu ya raia wa eneo hilo na kuharibu sehemu kubwa ya vituo vya huduma muhimu kwa raia kama vile shule, hospitali, misikiti na nyumba za raia.

Tangu kuwekwa kwa kizuizi hicho mwaka wa 2007, mamlaka za Israel zilizuia kuingia kwa bidhaa muhimu za Gaza kwa kisingizio kwamba zitakuwa na matumizi ya kiraia na kijeshi kama vile vifaa vya ujenzi, vifaa vya matibabu, na baadhi ya bidhaa za kilimo.

Mzingiro haramu wa utawala dhalimu wa Israel umepelekea Ukanda wa Gaza utajwe  kuwa  gereza kubwa zaidi la wazi kuwahi kushuhudiwa duniani huku wakazi wake wakiendelea kutaabika na matatizo mbalimbali ikiwa ni natija ya  mzingiro huo wa kiuchumi. 

3482300

Habari zinazohusiana
captcha