IQNA

Bahrain yahadaa walimwengu kwa mashindano ya Qur'ani na Formula One

10:11 - April 06, 2014
Habari ID: 1390961
Utawala wa kiimla wa Aal Khalifa nchini Bahrian unahadaa walimwengu na kujaribu kuficha jinai zake dhidi ya watu wa nchi hiyo kwa kuandaa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani na pia mashindano ya magari ya Formula One.

Kwa mujibu  wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA,Wizara ya Auqaf na Masuala ya Kiislamu Bahrain Jumanne iliyopita ilianza mashindano ya kimataifa ya Qur'ani kwa njia ya intaneti ili kujaribu kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusu jinai zake dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Aidha Habari kutoka nchini Bahrain zinaeleza kuwa askari usalama na jeshi la nchi hiyo wanashirikiana kwa karibu ili kukandamiza maaandamano makubwa ya malalamiko ya wananchi dhidi ya utawala wa nchi hiyo huku mashindano ya magari ya Formula One yakikaribia kufanyika nchini humo.
Habari zinasema kuwa jana Alkhamisi askari hao walivunja kwa nguvu za ziada maandamano ya wananchi waliokuwa wakishiriki katika mazishi ya Hussein Sharaf mmoja wa waandamanaji aliyeuawa siku ya Jumanne katika maandamano.
Ukandamizaji huo wa askari usalama na jeshi la Bahrain umeongezeka katika hali ambayo askari usalama wameongeza vituo vya ukaguzi na upekuzi katika miji tofauti ya nchi hiyo na hasa katika mji mkuu Manama, kwa kisingizio cha kuimarisha usalama wakati wa kufanyika mashindano ya Formula One. Ni wazi kuwa watawala wa Bahrain wana lengo la kuzidisha hali ya hofu, woga na wasiwasi miongoni mwa wananchi wa Bahrain ili kuwafanya wasitishe maandamano yao ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka mitatu sasa kwa lengo la kuung'oa madarakani utawala unaoendelea kukanyaga haki zao za kimsingi bila kujali lolote. Kwa kuandaa mashindano ya Formula One, bila shaka utawala wa Manama una lengo la kuwadhihirishia walimwengu sura bandia ya uanadamu kwa upande mmoja na wakati huohuo kujaribu kuonyesha kuwa hali ya usalama nchini humo ni shwari na isiyotia wasiwasi, kwa upande wa pili. Hali hiyo imewafanya wananchi wa Bahrain nao wazidishe harakati zao za kuvunja njama hiyo na kudhihirisha sura halisi ya unyama wa utawala huo.
Kuhusiana na suala hilo, Jumuiya ya al-Wifaq imewataka wananchi kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika maandamano ya kupinga kufanyika mashindano ya Formula One nchini humo. Wakati huohuo, Muungano wa Vijana wa Februari 14 umewataka wafuasi wao washiriki kwa wingi katika maandamano ya kupinga mashindano yaliyotajwa ambayo wameyapa kuwa ni mashindano ya 'Formula Damu.' Wananchi wa Bahrain wanapinga vikali kufanyika kwa mashindano hayo nchini humo kutokana na kuwa yanaandamana na udikteta na ukandamizaji mkubwa wa watawala wa nchi hiyo dhidi yao. Vyama na makundi ya upinzani ya Bahrain yanakosoa mashindano hayo kwa kusema kuwa yanaandaliwa na watawala wa Manama kwa lengo la kufunika jinai zinazotekelezwa na watawala hao dhidi yao. Tokea tarehe 14 Februari 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya amani ya wananchi wanaopigania haki zao za kimsingi za kutetea uhuru na demokrasia. Lakini badala ya kuheshimu haki hizo, utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukishirikiana kwa karibu na utawala mwingine wa kidhalimu wa Saudi Arabia pamoja na askari wengine wa kigeni katika kuwakandamiza wananchi hao.
Kuhusiana na suala hilo, Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limesema kuwa utawala wa Bahrain unaandaa mashindano hayo kwa lengo la kufunika jinai unazozitekeleza dhidi ya wananchi wake. Umesisitiza kuwa haki ya kufanya maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain inapasa kuheshimiwa kikamilifu na utawala wa Manama.
1390358

Kishikizo: bahrain qur'ani
captcha