IQNA

Amnesty yalaani kuhukumiwa kifo Morsi

10:53 - May 17, 2015
Habari ID: 3304307
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani hukumu ya kifo dhidi ya rais wa zamani wa Misri Mohammad Morsi na kusema kesi hiyo haikuzingatia taratibu za mahakama.

Amnesty International katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika Said Boumedouha amesema, 'kwa kuzingatia kuwa Morsi alishikiliwa kwa miezi kadhaa bila kuwepo usimamizi wa mahakama na pia ukweli kuwa hakuwa na wakili wakati wa kesi yake ni mambo ambayo yanapelekea kesi dhidi yake kuwa batili na isiyo na utaratibu.'

Amesema hukumu hiyo ya kifo ni ishara ya wazi ya kukiukwa haki za binadamu.

Aidha afisa huyo wa Amnesty International ameitaja kuwa ya kimaonyesho hatua ya aji Shaaban el-Shami  aliyesoma hukumu hiyo ya Morsi kusema uamuzi wa mwisho kuhusu kuitekeleza au kutoitekeleza utatolewa na Mufti Mkuu wa Misri.

Jana Mohammad Morsi alihukumiwa kifo na mahakama moja ya Cairo baada ya kupatikana na hatia ya kuhatarisha usalama wa taifa kwa kuikabidhi serikali ya Qatar siri za nchi. Aidha amepatikana na hatia ya kutoroka gerezani wakati wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani dikteta wa muda mrefu wa Misri Hosni Mubarak mwaka 2011.

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi, aliyempindua Morsi, analaumiwa kwa kuwakandamiza wapinzani hasa viongozi na wafuasi wa Ikhwanul Muslimin.

Morsi anahukumiwa kifo katika hali ambayo miezi michache iliyopita mahakama ya Misri ilimuondoa hatiani dikteta wa zamani Hosni Mubarak ambaye alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuua mamia ya wandamanaji katika mwamko dhidi ya utawala wake mwaka 2011. Punde baada ya hukumu ya dhidi ya Morsi kutangazawa, watu waliokuwa na silaha wamewapiga risasi na kuwaua majaji watatu  katika mji wa El Arish ulio katika eneo linalokumbwa na machafuko la Rasi ya Sinai.../em

3304216

captcha