IQNA

Wanazuoni wa Uislamu wakutana Misri kujadili ‘fatwa za misimamo mikali’

20:32 - August 18, 2015
Habari ID: 3345846
Wanazuoni wa Kiislamu leo wamemaliza kikao chao Misri ambapo wamejadili ‘fatwa za misimamo mikali’ ambazo zimekuwa zikitolewa na makundi ya kigaidi hasa kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS).

Kongamano hilo la siku mbili limehudhuriwa na mamufti, ambao wanatambuliwa kama wafasiri wa sheria za Kiislamu katika aghalabu ya nchi za Kiislamu pamoja na wanazuoni wengine wa Kiislamu kutoka nchi mbali mbali duniani. Ibrahim Negm mshauri wa Ibrahim Abdel-Kari Allam, Mufti Mkuu wa Misri amesema: “Lengo la kongamano hili ni kuleta umoja katika kauli za mamufti kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika eneo na duniani kutokana na fatwa zenye misimamo mikali na makundi ambayo hutoa kauli kwa jina la Uislamu.” Ameongeza kuwa kongamano hilo limejadili njia za kuanzishwa makao makuu ya mamufti ili kubatilisha fatwa za misimamo mikali sambamba na kutoa mafunzo kwa mamufti. Amesema kongamano hilo pia limejadili ‘stratijia mpya kwa ajili ya Waislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi ili waweze kukabiliana na fikra zenye misimamo mikali. Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar Sheikh Ahmed el-Tayeb ametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali kukabiliana na fatwa za watu wenye misimamo mikali. Mkutano huo umefanyika Cairo huku kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS likiendeleza ukatili Iraq, Syria, Misri na Libya. Aidha wakufurishaji wenye misimamo mikali wa makundi kama vile Boko Haram na Al Shabab wamekuwa wakieneza ukatili wao Afrika Magharibi na Mashriki.../mh

3345663

captcha