Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi (Jumatano) mjini Tehran aliponana na familia za mashahidi wa Mina
na wa Msikiti Mtakatifu wa Makkah. Aliongeza kuwa, kutokuwa na uwezo
ukoo wa Aal Saud wa kusimamia Hija kulikopelekea kutokea matukio hayo mawili ya kusikitisha mwaka jana katika msimu wa Hija, kwa
mara nyingine tena kumethibitisha namna mti huo khabithi uliolaaniwa
usivyo na ustahiki wa kusimamia na kuendesha Haram Mbili Tukufu za
Makkah na Madina. Amesisitiza kuwa: Kama Aal Saud wanasema kweli ya
kwamba hawakuwa na makossa katika tukio hilo, basi waruhusu kuundwe tume
ya kutafuta ukweli ya Kiislamu na kimataifa, ili iweze kuchunguza kwa
karibu jambo hilo na kuwaonesha walimwengu uhakika wake.
Ayatullah
Udhma Khamenei amesema kuwa, kuonana familia za mashahidi wa Mina na wa
Masjidul Haram kunakumbushia tukio chungu la mwaka jana na kuongeza
kuwa: Tukio la Mina lililopelekea kupoteza maisha mahujaji wengi
wakiwemo wa Kiirani wakiwa katika ibada na katika midomo yenye kiu,
chini ya jua kali, ni tukio la kusikitisha mno ambalo si rahisi
kusahaulika. Tab'an tukio hilo lina vipengee mbali mbali vya kuweza
kutumiwa kuwaamsha watu kisiasa, kijamii, kimaadili na kidini na inabidi
vipengee hivyo visisahauliwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu aidha amesema: Lilikuwa ni jambo zito sana kwa familia za
mahujaji kusikia habari ya kufariki dunia wapendwa wao na kupokea maiti
za jamaa za hao mwaka jana, lakini katika upande wa pili wa msiba huo,
kuna jambo jengine nalo ni kujua kwamba, wapendwa hao ni sawa na
mashahidi walioko chini ya kivuli cha maghufira, rehema na neema za
Mwenyezi Mungu na hilo linazipa utulivu na kuzifariji nyoyo za wafiwa.
Baada
ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kuuawa shahidi karibu
mahujaji elfu saba mwaka jana katika maafa ya Mina na kutoa lawama kali
akisema, kwa nini nchi na tawala zilizopoteza watu wao katika tukio
hilo, hazioneshi radiamali yoyote?
Amesema, hatua ya viongozi wa nchi
na maulamaa na wanaharakati wa kisiasa na wasomi na watu wenye vipawa
katika ulimwengu wa Kiislamu kunyamazia kimya suala la kuuawa shahidi
mahujaji elfu saba wasio na hatia, ni mtihani mkubwa kwa umma wa
Kiislamu na kuongeza kuwa: Kutoguswa na kutoonesha hisia zozote mbele ya
maafa mazito na yaliyosababisha huzuni kubwa kama ya Mina, ni msiba
mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi
ya Kiislamu aidha amesema, kitendo cha watawala wa Kisaudi cha kukataa
hata kuomba radhi kwa maneno tu ni jeuri iliyopindukia mipaka na ni
kukosa kwao haya na kuongeza kuwa: Hata kama tujaalie tukio hilo
halikufanyika kwa makusudi, lakini wa kulaumiwa kwa kosa hilo ni kundi
la watawala wa kisiasa wa nchi hiyo ambao wameshindwa kuweka mipango
madhubuti ya kusimamia vizuri amali ya Hija.
Ayatullah Udhma Khamenei
ameendelea na hotuba yake mbele ya majimui ya familia zenye majonzi za
mashahidi wa Mina kwa kuuliza swali muhimu akisema: Wakati utawala
fulani unaposhindwa hata kuwasimamia wageni wa Mwenyezi Mungu ambao
kwenda kwao Hija kuna pato zuri kwa utawala huo, kuna dhamana gani ya
kutojikariri maafa kama ya Mina wakati inapotokezea hali kama ya huko
nyuma?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa:
Taifa la Iran limesimama kishujaa kukabiliana na ujahili na upotofu wa
ukoo wa Aal Saud na linaendelea kubainisha kwa uwazi misimamo yake ya
haki inayotiwa nguvu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na inabidi mataifa
na nchi nyingine duniani zisimame kishujaa kukabiliana na ukoo huo wa
Aal Saud.
Amesema, kushindwa Wasaudia kusimamia vizuri amali ya Hija
na ukosefu wa usalama wanaobebeshwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah
kwa hakika ni jambo linaloonesha kuwa utawala huo wa Aal Saud hauna
ustahiki wa kusimamia Haram Mbili Tukufu na inabidi uhakika huo uenezwe
na kubainishwa vilivyo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma
Khamenei amesema, kipengee kingine kinachohusiana na tukio la Mina, ni
kimya cha kutisha kilichoonesha na watu wanaodai kulinda haki za
binadamu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia makelele ya kisiasa na kipropaganda
ya mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kuhusiana na utekelezaji
wa baadhi ya maamuzi ya mahakama katika baadhi ya nchi na kuongeza
kuwa: Kunyamazia kimya tena vibaya sana uzembe wa utawala fulani
ulioshindwa kutekeleza vizuri majukumu yake na kupekekea watu elfu saba
kufa kidhulma tena bila ya hatia, kunazidi kudhibitisha uongo wa watu
hao wanaodai kutetea haki za binadamu duniani na kwamba wale watu ambao
wana tamaa na mashirika ya kimataifa kama hayo, wanapaswa kupata funzo
kutoka katika tukio hilo chungu.
Ayhatullah Udhma Khamenei amesema,
kuundwa tume ya kutafuta ukweli ni miongoni mwa kazi za wajibu na za
dharura zinazopaswa kufanywa na nchi za Kiislamu na wale wanaodai
kutetea haki za binadamu duniani. Ameongeza kuwa, baada ya kupita mwaka
mzima tangu lilipotokea tukio hilo la kuhuzunisha mno, utafiti
uliofanywa kuhusu nyaraka na ushahidi mbali mbali wa video, sauti na
maandishi, umefichua kwa kiwango kikubwa uhakika wa tukio hilo.
Vile
vile amewahimiza viongozi wa Iran kulipa uzito mkubwa suala kufuatilia
uundwaji wa kama ya kutafuta ukweli na kuongeza kuwa: Kama Aal Saud wana
yakini na madai kuwa hawana makosa katika tukio la Mina, basi wasifumbe
midomo ya watu kwa kuwahonga fedha, na waruhusu kuundwa tume ya
kutafuta ukweli ili kulichunguza kwa uhuru na kwa karibu suala hilo.
Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya
hotuba yake kwamba wanaouunga mkono utawala wa Aal Saud ni washiriki wa
jinai za utawala huo katika maafa ya Mina na kuongeza kuwa: Utawala usio
na huruma wa Aal Saud kwa uungaji mkono wa Marekani, umesimama
kukabiliana na Waislamu kwa jeuri kubwa na unamwaga damu za Waislamu
katika nchi za Yemen, Syria, Iraq na Bahrain, hivyo Marekani na waungaji
mkono wote wa Riyadh ni washiriki wa jinai za Aal Saud.
Ayatullah
Udhma Khamenei ameashiria pia namna mashirika ya kipropaganda ya
vibaraka wa Saudia yanayofanya kila njia kujaribu kuzihusisha jinai za
Mina na hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni au
ugomvi baina ya Waarabu na wasio Waarabu na kuongeza kuwa: Wanaowasaidia
watawala wa Saudi Arabia katika propaganda wanakariri-kariri na
kurudia-rudia madai ya uongo wakati ambapo wengi wa mahujaji elfu saba
waliouawa shahidi huko Mina, ni Waislamu wa Kisuni licha ya kuweko pia
mahujaji wengi wa Iran waliouawa shahidi kwenye maafa hayo.
Amesema:
Ukoo wa Aal Saud na magenge ya magaidi makatili yalioanzishwa na kutiwa
nguvu na wao wenyewe yanawaua kwa umati Waarabu katika nchi za Yemen,
Syria na Iraq, hivyo tofauti na propaganda za kikhabithi zinazoenezwa na
Wamagharibi, Wasaudia si watetezi na wala si walinzi wa Waarabu na
kwamba tukio la Mina halina uhusiano wowote na mvutano wa kupandikiza
unaodaiwa kuwepo baina ya Waarabu na wasio Waarabu.
Kiongozi Muadhamu
wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Uhakika wa jambo hilo ni
kwamba, Wasaudia wanaochukiza, ni kundi ndani ya ulimwengu wa Kiislamu
ambalo baadhi yao kwa kujua na baadhi yao kwa kutojua, wanawafanyia
vitendo vya kiadui Waislamu na kwamba ulimwengu wa Kiislamu una wajibu
wa kusimama kidete kukabiliana nao na vile vile utangaze kujibari na
kuwa mbali kwake na mabwana wa Wasaudia yaani Marekani na Uingereza
makhabithi.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Sayyid Ali
Khamenei amezitaka taasisi na vyombo mbali mbali nchini Iran ikiwemo
Wizara ya Mambo ya Nje, Taasisi ya Biitha, Taasisi ya Hija na Taasisi ya
Mashahidi, zitekeleze vilivyo na zifuatilie kwa uzito mkubwa majukumu
yao kuhusiana na tukio kubwa la Mina.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi
Asgar, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) katika masuala ya
Hija na Ziara ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kuwakumbuka mashahidi
wa Septemba 8, 1978, na pia mashahidi wa Ijumaa ya umwagaji damu huko
Makkah iliyotokea mwaka 1366 Hijria Shamsia (Agosti 2, 1987) na
mashahidi wa Hija ya mwaka jana na kusema kuwa, maafa mawili makubwa ya
Mina na lile la ndani ya Masjidul Haram, yaliigeuza furaha ya Hija kuwa
msiba na kuwatumbukiza watu na familia zao kwenye majonzi makubwa.
Hujjatul
Islam Walmuslimin Qadhi Asgar amegusia pia namna Wasaudia
wanavyokwamisha juhudi za kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu maafa
hayo na kusema kuwa, Taasisi ya Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu na Taasisi ya Hija ya Iran zimekusanya ushahidi
mbali mbali uliotolewa kuhusiana na maafa hayo na kwamba imeshirikiana
na wanasheria kugundua njia za kulifuatilia jambo hilo katika taasisi za
kisheria za kimataifa na kamwe hazitaruhusu suala la Mina lisahauliwe.
Naye
Hujjatul Islam Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi
Mtawala ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya
Kujitolea katika Njia ya Haki ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na
hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kuhusu matukio ya Mina na Masjidul
Haram na kusema: Maafa ya kutisha na kutia majonzi ya Mina yametokea
kutokana na uendeshaji mbaya na uanagenzi wa ukoo wa Aal Saud.
3528593