IQNA

Israel imeua watoto 3,000 Wapalestina

19:12 - June 02, 2017
Habari ID: 3471004
TEHRAN (IQNA)-Jeshi la Utawala haramu wa Israel limeua shahidi watoto zaidi ya 3,000 Wapalestina tangu ulipoanza mwamako wa pili wa Wapalestina maarufu kama Intifadha mwezi Septemba 2000.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Alhamisi hii na Wizara ya Habari ya Palestina  kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuwalinda Watoto ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni Mosi, mbali na watoto hao 3,000  kuuawa shahidi, wengine zaidi ya 13 elfu wamejeruhiwa na wanajeshi  makatili wa utawala haramu wa Israel.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, watoto wasiopungua 72 wameuliwa shahidi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwezi Oktoba 2015, wakati ilipoanza Intifadha ya Tatu ya Quds.

Kadhalika ripoti hiyo ya Wizara ya Habari ya Palestina imebainisha kuwa, watoto zaidi ya 12 elfu wa Kipalestina wametekwa nyara na askari wa Israel na kuzuiliwa chini ya mazingira magumu, katika kipindi cha miaka 17 iliyopita.

Harakati ya Kimataifa ya Kuwalinda Watoto mwaka jana iliripoti kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanawauwa kwa makusudi watoto wa Kipalestina.

Katika kutekeleza siasa zake za kibaguzi na kutaka kungamiza kizazi cha Palestina, Israel inatekeleza siasa za kuua watoto wadogo. Utumiaji mabavu wa Israel dhidi ya watoto wa Palestina bila shaka unaenda kinyume na sheria za kimataifa na hasa kipengee cha 16 cha hati ya haki za watoto, ambacho kinapiga marufuku kuamiliana kimabavu na watoto.

Mbali na hayo muamala wa kimabavu wa askari wa Kizayuni dhidi ya watoto wa Palestina unapingana wazi na hati nne za Geneva ambazo zinasisitiza kulindwa haki za watu ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na hasa kuheshimiwa haki za watoto.Israel imeua watoto 3,000 Wapalestina

Hii ni katika hali ambayo ripoti tofauti za kimataifa zinasema kwamba watu wa matabaka tofauti ya Palestina wakiwemo watoto, wanakabiliwa na jinai na vitendo vya mabavu na mateso vya utawala wa Kizayuni ambao hautambui mipaka yoyote ya sheria. Ukiukaji wa haki za watoto wa Palestina unaofanywa na utawala wa Israel hauna mwisho na utawala huo unadumisha jinai hizo dhidi ya watoto hao bila ya kuwa na hofu yoyote ya kufikishwa mbele ya vyombo vya mahakama wala kuwajibishwa na jamii ya kimataifa.

3463005

captcha