IQNA

Waasi wa ADF waua 16 mashariki mwa DRC

22:54 - February 15, 2021
Habari ID: 3473651
TEHRAN (IQNA)- Wati 16, wakiwemo raia 13 na askari watatu wameuawa jimboni Ituri Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokraisia ya Kongo (DRC) kufuatia hujuma ambayo imetekelezwa na waasi wa ADF kutoka nchi jirani ya Uganda.

 Mbunge wa jimbo hilo Iracan Gratien, amesema waasi walishambulia kijiji cha Ndala wilayani Irumu jana Jumapili na kuchoma moto kanisa moja.

 

Duru toka eneo la tukio zinasema, waasi hawa walianza kwanza kushambulia vizuizui vya jeshi la nchi hiyo .

Kwa miaka kadhaa sasa, majimbo yanayokuwa na madini yanakabiliwa na uasi huku wachambuzi wengi wakikosoa wafanyabiashara kuwa sehemu ya vurugu hizo ili wauze madini kwa njia isiyo halali.

Jana pia, mji mkuu wa jimbo la madini la haut-Katanga Lubumbashi, lilishambuliwa na waasi wengine ambao walijaribu kuchukuwa udhibiti wa mahali pa kuhifadhi silaha na kambi mbili za vikosi maalum vya ulinzi wa jimbo hilo.

Jeshi la taifa lilitangaza kuwa waasi 12 waliuawa huku wakipoteza wanajeshi wao watatu pamoja na mtoto mmoja wa askari.

Kundi la ADF linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa kundi la ADF linashirikiana na makundi ya kigaidi ya kimataifa kama vile ISIS au Daesh. Hatahivyo wataalamu wa Umoja wa Mataifa hadi sasa hawajaweza kuthibitisha kuwepo uhusiano baina ya makundi hayo mawili.

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.

3473985

Kishikizo: congo adf waasi
captcha