IQNA

Sayyid Nasrallah: Iran imethibitisha kuwa ni mshirika mkweli

13:09 - October 08, 2021
Habari ID: 3474395
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kuhusu matukio ya karibuni kabisa ya kisiasa ya nchi hiyo na eneo.

Katika mazungumzo yake hayo na Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ametilia mkazo juu ya misimamo thabiti ya Iran kuhusiana na Lebanon na uungaji mkono wake, kusimama kwake imara na kuwa bega kwa bega na nchi hiyo katika nyuga zote.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah amesema, Iran imethibitisha kuwa ni mshirika mkweli na rafiki mwenye muamana, ambaye hawaachi mkono na peke yao marafiki zake; na akaishukuru Jamhuri ya Kiislamu kwa kusimama imara na bega kwa bega na serikali, wananchi na muqawama wa Lebanon tangu miongo kadhaa nyuma hadi hivi sasa.

Katika safari yake ya kwanza nchini Lebanon akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir- Abdollahian aliwasili mjini Beirut usiku wa kuamkia jana na akakutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa nchi hiyo akiwemo Rais Michel Aoun, Spika wa Bunge Nabih Berri, Waziri Mkuu Najib Mikati na Waziri wa Mambo ya Nje Abdallah Bou Habib juu ya masuala ya pande mbili na ya kieneo.

Kabla ya kuelekea Beirut, Amir-Abdollahian alikuweko mjini Moscow, ambako alikutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov.

3475940/

captcha