IQNA

Mazungumzo ya jeshi na wanasiasa Sudan kuhusu kugawana madaraka

11:39 - November 04, 2021
Habari ID: 3474512
TEHRAN (IQNA)- Jeshi Sudan ambalo limenyakua uongozi wa nchi hiyo kufuatia mapinduzi ya hivi karibuni linaendelea na mazunguumzo na Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu aliyeondolewa madarakani.

Baadhi ya duru zilizo karibu na Waziri Mkuu huyo aliyepinduliwa zimedokeza kuwa, mazungumzo yanayoendelea sasa yanajadili uwezekano wa kiongozi huyo kurejea kuiongoza serikali ya mpito na kwamba, kumepigwa hatua nzuri katika mazungumzo hayo.

Kumekuwepo na taarifa zinazogongana kuhusiana na mazungumzo hayo baada ya kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Saudi Arabia cha al-Arabiya kuripoti kwamba, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok ameafiki kurejea kuiongoza serikali ingawa hakikuweka wazi vyanzo vya taarifa hiyo.

Ripoti nyingine zinanukuu baadhi ya vyanzo vilivyokutana na Waziri Mkuu huyo wiki iliyopita kwamba, anataka wafungwa wa kisiasa waachiwe huru kama moja ya masharti ya kukubali kuingia kwenye mazungumzo ya kina ya kuongoza tena serikali ya Sudan.

Kulingana na Umoja wa Mataifa juhudi za kusaka suluhu ya mzozo huo zimekuwa zikiendelea kwa siku kadhaa na kwamba, pande zote zimeonyesha nia ya kujinasua kwenye mzozo huo wa kisiasa.

Jumatatu ya tarehe 25 Oktoba majenerali wa jeshi la Sudan walifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Mapinduzi hayo ya kijeshi yalifanyika chini ya mwezi mmoja tu kabla ya muda aliopaswa Jenerali al Burhan kukabidhi uongozi wa Baraza la Utawala linaloendesha nchi, kwa viongozi wa kiraia, hatua ambayo ingelipunguza nguvu za jeshi za kushikilia madaraka.

3476333

Kishikizo: sudan jeshi mapinduzi
captcha