IQNA

Iran yakaribisha hatua ya Algeria kwa kupinga Israel kuwa mwanachama Umoja wa Afrika

20:26 - November 12, 2021
Habari ID: 3474548
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua ya hivi karibuni ya Algeria kupinga utawala haramu wa Israel kupewa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Hussein Amir-Abdollahian aliyasema hayo Alhamisi katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Algeria Ramtane Lamamra na kuongeza kuwa, hatua ambayo imechukuliwa na Algeria imejengeka katika msingi wa hekima na mantiki.

Amir-Abdollahian amesema: “Hatua mliyochukua pamoja na msimamo wa Algeria kuhusu Syria kurejea katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni hatua za kupongezwa.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameelezea matumaini yake kuwa katika kikao kijacho cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, hatua muhimu zitachukuliwa kwa maslahi ya Umma wa Kiislamu.

Kuhusu uhusiano wa kirafiki baina ya Iran na Algeria, Amir-Abdollahian ameelezea matumaini kuwa uhusiano baina ya nchi hizi mbili utaimarika zaidi.

Kwa upande wake, Lamamara amemualika Amir-Abdollahian kutembelea Algeria huku akisisitiza umuhimu wa kuundwa kamati ya kufuatilia masuala ya uhusiano wa pamoja baina ya nchi mbili.

Ikumbukwe kuwa mwezi Agosti, Algeria ilipinga vikali hatua ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuupa utawala haramu wa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika umoja huo. Algeria imeonya kuwa, hatua hiyo hatimaye itapelekea kuvunjika Umoja wa Afrika.

/84537493

captcha