IQNA

Rais wa Iran asisitiza kuhusu mkakati wa kuwa na uhusiano mwema na nchi jirani

15:56 - December 11, 2021
Habari ID: 3474666
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera za ujirani mwema na kuwa na uhusiano na majirani ili kusambaratisha vikwazo ni mkakati wa kistratijia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumamosi mjini Tehran alipokutana na mabalozi pamoja na wawakilishi wa Iran nje ya nchi kwa lengo la kujadili uhusiano na nchi jirani. Raisi ameongeza kuwa: "Kwa kuzingatia uwezo uliopo ndani ya Iran, tunaweza kuimarisha mabadilishano ya kibiashara na nchi jirani na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ina nafasi kubwa katika uga huu."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mikakati miwili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kusambaratisha na kuondolewa vikwazo na kusema: "Baadhi walikuwa wakisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo na wengine walikuwa wanadai kuwa Iran haishiriki katika mazungumzo kwa azma imara au haina mpango maalumu; lakini Jamhuri ya Kiislamu imeshiriki katika mazungumzo kwa nguvu na imewasilisha matini na kwa kuwasilisha matini ya mapendekezo imeonyesha kuwa ina azma imara katika mazungumzo."

Hali kadhalika Rais Raisi amesema iwapo upande wa pili kweli unataka kuiondolea Iran vikwazo vya kidhalimu basi mapatano mazuri yatafikiwa na kwa yakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka mapatano mazuri.

Rais wa Iran aidha amesema baadhi ya nchi zinajaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kuufanya utawala huo ukaribie mipakaya eneo jambo ambalo halitakuwa na faida kwa nchi za eneo.

Raisi amesema Iran inazitakia mema nchi za eneo na kuongeza kuwa: "Ushirikiano wa nchi za eneo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaweza kusaidia katika kuimarisha usalama, amani na utulivu katika eneo."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema matatizo ya Afghanistan yanatokana na uwepo wa madola ajinabi nchini humo na kuongeza kuwa, tokea wakati askari wa NATO na Marekani walipoingia Afghansitan, nchi hiyo haijawahi kushuhudia siku njema na kuongeza kuwa Wamarekani waliibadilisha Afghanistan kuwa kitovu cha mihadarati.

4020079

captcha