IQNA

Wapalestina walaani Australia kwa kuiita Hamas kundi la 'kigaidi'

20:57 - February 19, 2022
Habari ID: 3474946
TEHRAN (IQNA)- Makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina yamekosoa vikali kitendo cha Australia cha kuitambua harakati ya muqawama ya HAMAS kuwa ni kundi la kigaidi.

Khalid al-Battash, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul Islami amesema hatua hiyo ya kikatili inaenda sambamba na matakwa ya Tel Aviv ya kutaka kuharamishwa juhudi zote za kukombolewa ardhi za Wapalestina na kupewa haki zao za msingi.

Nayo Kamati ya Muqawama ya Palestina (PRC) imesema hatua hiyo inaonesha wazi namna Australia ilivyo na misimamo hasi dhidi ya Wapalestina, na inavyoiunga mkono Israel licha ya utawala huo haramu kuwaua na kuwafanyia kila aina ya jinai wananchi madhulumu wa Palestina. 

Wakati huohuo, Harakati ya Mujahideen ya Palestina imesema kitendo hicho cha Australia ni muendelezo wa sera za Wamagharibi za uvamizi na ukaliaji kwa mabavu wa ardhi za Wapalestina kinyume cha sheria za kimataifa.

Kadhalika Jukwaa la Kidemokrasia la Ukombozi wa Palestina (DFLP) limesema hatua ya  Australia ya kuitambua harakati ya muqawama ya HAMAS kuwa ni kundi la kigaidi ni kubariki jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Nacho Chama cha Watu wa Palestina (PPP) kimesema Australia imetangaza wazi kiapo chake cha utiifu kwa Israel na sera za uvamizi za utawala huo pandikizi.

Radiamali hizo za makundi ya muqawama ya Palestina zimetolewa baada ya Karen Andrews, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia kutangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo itaiweka harakati ya HAMAS inayopigania ukombozi wa Palestina  katika orodha ya makundi ya kigaidi.

84654118

captcha