Kwa mujibu wa taarifa, takribani washiriki 40,000 kutoka nchi 80 walishiriki katika mchujo wa mashindano hayo kwa kutuma klipu za qiraa yao ya aya za Qur’ani Tukufu au adhana katika mashindano hayo yajulikanayo kama Otr Elkalam.
Mamlaka ya Tamasha Saudia imesema imetenga kiwango kikubwa zaidi cha zawadi katika mashindano ya Qur’ani duniani ambapo jumla ya zawadi zitakazotolewa zina thamani ya dola milioni 3.2.
Mshindi wa kwanza katika qiraa ya Qur’ani Tukufu atapata zawadi ya dola milioni 1.3 na mshindi mwenye sauti bora zaidi ya adhana atapata zawadi ya dola laki 5.3. Fedha zilizosalia zitawaendea washindi wengine sita.
Baada ya washiriki 40,000 kushiriki katika mchujo hatimaye washiriki 36 walifika katika fainali. Miongoni mwa waliofika fainali ni wawakilishi wa Saudi Arabia, Iran, Misri, Iraq, Algeria, Uturuki, Malaysia, Indonesia, Canada na Uingereza.