IQNA

Watu zaidi ya milioni 1.2 wametembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran

15:01 - May 01, 2022
Habari ID: 3475192
TEHRAN (IQNA) – Afisa wa Wizara ya Utamaduni ya Iran anasema malengo ya Maonyesho ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran yamefikiwa kwa usaidizi wa watu na mashirika.

Akizungumza na IQNA, Ali Reza Moaf, Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu anayeshughulikia Qur'ani na Etrat ambaye ni mkuu wa maonyesho hayo amesema waandaaji walikuwa na siku 40 pekee za kuandaa hafla hiyo mwaka huu ikilinganishwa na kipindi cha miezi sita katika miaka iliyopita.

Akiangazia idadi kubwa ya wageni katika maonyesho ya mwaka huu, alisema kushiriki kwa wingi katika maonyesho hayo ni ishara ya ustawi wa utamaduni..

Kulingana na takwimu zilizotolewa, zaidi ya watu milioni 1.2 walitembelea maonyesho hayo ya wiki mbili, alisema.

Aidha amebaini kuwa maonyesho ya  mwaka huu yamelenga kuzivutia familia, vijana na watoto, na kuongeza kuwa mkakati wa hafla hiyo ni kuigeuza na kuwa ya watu wote kwani Quran Tukufu ni ya watu wote.

Maonyesho ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran yalizinduliwa tarehe 16 Aprili katika Ukumbi wa Sala (Musalla) wa Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu- na yamemalizika 29 Aprili.

Maonyesho hayo huandaliwa kila mwaka na Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kati ya malengo muhimu ya maonyesho hayo ni  kukuza itikadi za Qur'ani na kuendeleza shughuli za Qur'ani kote Iran na katika nchi zingine duniani..

Maonyesho hayo yanaonyesha mafanikio ya hivi punde zaidi ya Qur'ani nchini humo pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kutangaza Kitabu hicho Kitakatifu.

4054046

captcha