IQNA

Jinai za Israel

Wanawake 16,000 Wapalestina wamekamatwa katika jela za Israel

17:09 - August 28, 2022
Habari ID: 3475694
TEHRAN (IQNA) - Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, utawala haramu wa Israel umewatia mbaroni zaidi ya wanawake 16,000 wa Kipalestina tangu mwaka 1967 huku mashirika ya haki yakionya kuhusu hali mbaya ya wafungwa wa kike katika jela za kuogofya za Israel.

Addameer, asasi isiyo ya kiserikali ya Wapalestina ambayo inafuatilia jinsi wafungwa wa Kipalestina wanavyotendewa na imetoa ufichuzi huo na kusema: "Israel imewakamata zaidi ya wanawake 16,000 wa Kipalestina tangu 1967." Ripoti hiyo imeongeza kuwa mashirika mengi ya haki za binadamu yameripoti kuwepo unyanyasaji wa kikatili na udhalilishaji wa wafungwa wanawake wa Kipalestina wanapokuwa katika magereza ya Israel, ikiwa ni pamoja na kuteswa, kudhalilishwa kingono, kunyimwa kutembelea familia zao,  kukosekana huduma za matibabu na zikiwemo zinakuwa ni mbovu sana, na ukosefu wa elimu.

Shirika lisilo la kiserikali la Palestina pia limeashiria wanawake 32 wa Kipalestina wanaoteseka hivi sasa katika jela za utawala dhalimu wa Israel za Damon na Hasharon.

"Kuta ni baridi sana, vyumba vingi havina hewa ya kutosha, vina unyevunyevu, na vimejaa wadudu," alisema Nisreen Abu Kmail, mfungwa wa zamani huko Damon. "Jengo ni kuukuu, milango mingi ina kutu kutokana na unyevunyevu. Hakuna viti katika vyumba, na wasimamizi wa gereza wanawazuia wanawake kufunika sakafu na blanketi.”

Ripoti hiyo imeongeza kuwa akina mama wengine kumi wa Kipalestina waliojifungua watoto wao wakiwa kizuizini pia wanapitia matatizo makubwa katika jela ya Damon.

Zaidi ya wafungwa 7,000 wa Kipalestina kwa sasa wanazuiliwa katika takriban jela 17 za Israel. Mamia ya wafungwa, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wanazuiliwa bila kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imelaaniwa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu.

3480247

captcha