IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hujuma ya kigaidi la Shah Cheragh imeifedhehesha Marekani

21:38 - December 20, 2022
Habari ID: 3476275
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana na familia za watu waliouawa shahidi katika shambulio ya kigaidi la Haram ya Shah Cheragh AS mjini Shiraz na kusema kuwa, shambulio hilo limeifedhehesha Marekani na kuonesha unafiki wao na roho zao mbaya.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesema hayo leo Jumanne kwenye mazungumzo yake na familia za mashahidi wa tukio hilo na kuongeza kuwa, shambulio la kigaidi kwenye Haram hiyo limezitia majonzi nyoyo zetu sote lakini pia litabakia kwenye historia ya Iran na kufichua mikono iliyohusika na jinai hiyo yaani dola la kiistikbari la Marekani ambalo ndilo lililoliunda genge la kigaidi la Desh (ISIS).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, kuuliwa kigaidi wafanyaziara hao sambamba na matukio mengine ya kigaidi kumezidi kuwafedhehesha watenda jinai wa ISIS na waungaji wao wakuu yaani Marekani.  Vile vile kumezidi kufichua uongo na roho zao mbaya na unafiki wao ambapo wananyanyua juu bendera ya kupigania haki za binadamu lakini katika vitendo wanaunda na kuunga mkono magenge hatari ya kigaidi kama Daesh.

Aidha amezitaka taasisi za kiutamaduni na sanaa kuliakisi vizuri suala hilo kama zinavyoliakisi tukio la Ashura na masuala mengine ya kihistoria ili kulifikisha vizuri na kwa njia sahihi kwa vizazi vijavyo. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 26 Oktoba mwaka huu wa 2022, gaidi mmoja wa Daesh aliingia kwenye Haram toharifu ya Ahmad bin Musa maarufu kwa jina la Shah Cheragh katika mji wa Shiraz ambao ndiyo makao makuu ya mkoa wa Fars wa Iran na kuua shahidi na kidhulma watu 15 wakiwemo watoto wadogo wawili na kujeruhiwa wafanyaziara wengine 30.

 4108383

captcha