IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Ayatullah Sistani alaani hatua ya Uswidi kuruhusu vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu

14:47 - June 30, 2023
Habari ID: 3477215
Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marjaa wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq amelaani hatua ya Uswidi (Sweden) kuruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini humo na ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa vitendo vya kuvunjiwa heshima kitabu cha Waislamu cha Qur'ani Tukufu.

Ofisi ya Ayatullah Sistani imesema kuwa, Marjaa huyo amemuandikia barua Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na hatua ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko nchini Sweden tena kwa kibali cha polisi ya nchi hiyo.

Sehemu moja ya barua ya Ayatullah Sistani kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiifa inasema: Kuheshimu uhuru wa kusema, hakuwezi kuwa ndio idhini ya kitendo hiki cha fedheha cha kuvunjia heshima matukufu ya zaidi ya Waislamu bilioni mbili duniani.

Wakati huo huo, waandamanaji mjini Baghdad wamvamia ubalozi wa Sweden mjini humo kulalamikia kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na kutaka kutimuliwa mjini humo balozi wa taifa hilo la Ulaya.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iraq imemuita katika makao makuu ya wizara hiyo balozi wa Sweden na kumkabidhi malalalmiko yake ya kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran pia imemuita balozi wa Sweden mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko kama hayo pia. Mataifa ya Jordan na Imarati pia yamechukua hatua kama hiyo.

Katika upande mwingine, Rais Recep Tayyip Erdogan amelaani vikali kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na kukosoa vikali hatua ya mamlaka husika nchini humo ya kutoa kibali cha kutekelezwa kitendo kama hicho.

Katika upande mwingine Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa mwito wa kususiwa bidhaa za Sweden baada ya kushuhudiwa kwa mara nyingine kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika ardhi ya Sweden tena mara hii kikifanyika kwa kibali na ridhaa ya mamlaka husika katika nchi hiyo.

3484138

captcha