Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameyasema hayo alipohutubua makumi ya maelfu ya watu na wafanyaziara
katika Haram Takatifu ya Hadhrat Ali bin Musa Ridha AS, Imam wa nane wa
Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mtakatifu wa Mashhad kaskazini
mashariki mwa Iran. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, Marekani inataka
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isitishe uungaji mkono wake kwa
waliodhulumiwa katika eneo, taifa la Palestina, Ghaza, Yemen na Bahrain.
Amesisistiza kuwa, wao (mfumo wa kibeberu ukiongozwa na Marekani)
wameshindwa katika kadhia za Syria, Iraq na Palestina na wanaona
kushindwa kwao huko kumesababishwa na Iran. Ayatullah Khamenei
ameashiria ukuruba na kushirikiana baadhi ya nchi na serikali za eneo na
utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema wanataka Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran nayo iwe pamoja na utawala huo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesema matakwa ya Marekani kwa Iran yana maana kuwa, Jamhuri
ya Kiislamu iende sambamba na matakwa ya Marekani na hata iachane na
uwezo wake wa kujihami.
Ayatullah Khamenei ameashiria namna Marekani inavyoikosoa Iran kutokana na kufanyia majaribio makombora yake pamoja na mazoezi ya kijeshi na kusema, Marekani hufanya mazoezi ya kijeshi mara kwa mara katika Ghuba ya Uajemi kwa kushirikiana na mojawapo ya nchi za eneo katika hali ambayo eneo hili liko mbali sana na Marekani na pia pamoja na kuwa Washington haina jukumu lolote katika eneo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) baina ya Iran na madola sita yenye nguvu zaidi duniani na kusema, Marekani haijatekeleza ahadi zake katika mapatano hayo ya nyuklia na ingali inaendeleza vikwazo dhidi ya Iran. Ameongeza kuwa, harakati ya kimapinduzi na uchumi wa kimuqawama (kimapambano) ni nukta ambazo zitaiokoa Iran na kusisitiza kuwa, iwapo nukta hizo zitatekelezwa basi vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havitakuwa na taathira.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njia mbili za kuchagua kwa mtazamo wa mfumo wa kibeberu ambazo ni ima kusikilizana na Marekani au kustahamili daima mashinikizo ya Marekani na matatizo yatokanayo na mashinikizo hayo na kusema: "Kwa Uchumi wa Muqawama (mapambano); Hatua na Utekelezaji tunaweza kusonga mbele." Ayatullah Khamenei amesistiza kuwa, vijana wa Iran wanapaswa kufahamu kuwa iwapo watajitokeza katika medani na wakajiamini, Marekani na hata mkubwa zaidi ya Marekani hatoweza kufanya ghalati yoyote.