IQNA

Ikhwanul Muslimin Sudan: Kuanzisha uhusiano na Israel ni kuwasaliti Wapalestina

16:21 - October 09, 2020
Habari ID: 3473243
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Sudan amekosoa hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema, hatua hiyo ni usaliti kwa kadhia ya Palestina.

Dr. Adel Ali Allah amesema kuwa mataifa ya Kislamu ya Kiarabu yanaamini kuwa matukufu ya Kiislamu ya Palestina yanapasa kukombolewa haraka iwezekanavyo kutoka katika makucha ya utawala ghasibu wa Kizayuni. 

Kiongozi wa Ikhwanull Muslimin ya Sudan ameongeza kuwa: "Tawala za Kiarabu zinadhani kwamba zinapiga hatua na mfumo wa dunia lakini jambo hili si suala la Wayahudi wala Waarabu bali ni kadhia ya kukaliwa kwa mabavu ardhi. Nchi hizo ambazo zinafanya juhudi za kuanzisha uhusiano rasmi  na Israel ni tawala ambazo mifumo yake ya uongozi ni ya mtu binafsi na wananchi wao hawana haki yoyote ndani ya mifumo hiyo."

Dr. Ali Allah amesisitiza kuwa Marekani na nchi nyingine zinazounga mkono utawala ghasibu wa Israel zinajaribu kuiwekea Sudan mashinikizo ya kiuchumi na kuwadhihirishia wananchi taswira hii kwamba kuanzisha uhusiano na Israel kutatatua matatizo ya serikali ya Sudan. Lakini hizo zote ni njozi tupu na zisizo na ukweli wowote. 

Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain baada ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu; tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu zilisaini huko White mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala huo wa Kizayuni. Tukio hilo lilihudhuriwa na Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. 

3928184

captcha