IQNA

Ngome ya magaidi wa ISIS yasambaratishwa mjini Kabul

16:38 - October 05, 2021
Habari ID: 3474383
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Taliban nchini Afghanistan umetangaza habari ya kuuvunja mtandao wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo la kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.

Msemaji wa kundi la Taliban, Zabihullah Mujahid amesema Jumatatu kuwa, vikosi vya Taliban vimeshambulia ngombe ya ISIS kaskazini mwa kabul, kufuatia hatua ya wanachama wa kundi hilo la ukufurishaji kutekeleza hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti wa Eidgah jijini Kabul.

Watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi nje ya msikiti huo siku ya Jumapili.

Mujahid amesema wanachama wote wa genge la Daesh wameangamizwa katika operesheni ya jana usiku iliyofanywa na askari wa kikosi maalumu cha kundi la Taliban.

Msemaji huyo wa Taliban ameeleza kusikitishwa kwake na hujuma ya kigaidi ya Jumapili iliyolenga raia wa kawaida wakiwa katika eneo la ibada huko kaskazini mwa Kabul.

Mripuko mkubwa wa bomu ulisikika Jumapili adhuhuri nje ya msikiti wa Eidgah jijini Kabul, wakati wa Swala ya maiti ya mama ya Zabihullah Mujahid, ambaye ameteuliwa kuwa naibu waziri wa habari na utamaduni wa utawala wa Taliban.

4002493

captcha