IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Iran inataka vikwazo vyote viondolewe katika mazungumzo ya Vienna

17:05 - December 17, 2021
Habari ID: 3474687
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa msingi wa mazungumzo ya nyuklia JCPOA yanayofanyika mjini Vienna ni kuondolewa kwa mpigo vikwazo ilivyowekewa Iran.

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema, msingi mkuu wa mazungumzo ni kuondolewa vikwazo kwa mpigo na kukubali pande za Ulaya na Marekani kutekeleza majukumu yao; kwa hivyo inapasa upande wa pili katika mazungumzo ya JCPOA uthamini hatua ya Iran ya kushiriki katika mazungumzo licha ya wao kuhalifu ahadi na makubaliano.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ameongeza kuwa: ujumbe wa Iran umeingia kwenye medani ya mazungumzo kwa uthabiti na ubunifu ijapokuwa upande wa pili unafuata njia ya upotoshaji kwa kuchochea mivutano ndani ya Iran, kujaribu kuvuruga umakini wa timu yake ya mazungumzo na kupata maslahi zaidi katika mazungumzo, lakini hautafanikiwa.

Haj Ali Akbari amebainisha kuwa, wao wamehalifu makubaliano, kwa hiyo wathamini kufanyika mazungumzo hivi sasa; na msingi wa mazungumzo uwe  ni kuondoa vikwazo kwa mpigo na kukubali pande za Ulaya na Marekani kutekeleza majukumu yao na kuacha kuzungumzia mambo ya pembeni.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amegusia pia vitisho wanavyotoa baadhi ya maafisa wa nchi za Magharibi vya kuanzisha chokochoko dhidi ya Iran na akasema: misimamo ya baadhi ya nchi za Magharibi katika jambo hili inafanana zaidi na dhihaka, kwani wao wenyewe wanajua kwamba hawathubutu kufanya upuuzi wowote.

Haj Ali Akbari ameongezea kwa kusema: tuna matumaini kuwa, katika diplomasia pia wanadiplomasia wa Kiirani watapata ushindi unaostahiki; hata hivyo kuondolewa vikwazo ni upande mmoja wa kadhia, lakini suala la msingi ni kuvunja nguvu za vikwazo; na kuvivunja nguvu vikwazo kutawezekana tu kwa kutegemea uwezo wa ndani.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake ya Sala ya Ijumaa, khatibu wa leo wa sala hiyo ameashiria pia kuwadia masiku ya kuomboleza kufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahraa AS na akasema: Inapasa tumtambue Bibi Fatima AS kuwa ni mwasisi wa Jihadi.

4021471

captcha