IQNA

Jinai za Israel

Hamas yapongeza Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina kumiliki maliasili

21:14 - December 16, 2022
Habari ID: 3476256
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya Mappambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilikaribisha kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa linalotambua mamlaka ya Palestina juu ya maliasili katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) siku ya Alhamisi lilipitisha azimio la kutangaza kwamba Wasyria na Wapalestina wana mamlaka juu ya maliasili zao katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel katika Miinuko ya Golan ambayo ni ya kistratijia na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwemo al-Quds Mashariki.

Baraza Kuu lilipitisha azimio hilo ambapo nchi 159 ziliunga mkono, 8 zilipinga na 10 hazikuunga mkono.

Utawala wa Israel, Marekani, Kanada, Chad, Visiwa vya Marshall, Mikronesia, Nauru, na Palau ndio waliopiga kura kupinga azimio hilo.

"Kwa azimio hilo, Baraza liliitaka Israel, ambayo inakalia kwa mabavu Palestina, kusitisha uporaji, uharibifu, na kuhatarisha maliasili katika eneo linalokaliwa la Palestina," UN ilisema.

Azimio hilo pia linataka kusitishwa vitendo vyote vinavyodhuru mazingira, vikiwemo vitendo vinavyofanywa na walowezi wa Israel kwa kutupa taka za kila aina katika Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

UNGA ilisema hatua kama hizo ni tishio kubwa kwa maliasili ya idadi ya watu, haswa rasilimali za maji na ardhi, na kutishia mazingira na afya ya raia na vifaa vyao.

Abdel-Latif Al-Qanou, msemaji wa Hamas amepongeza hatua hiyo na kuutaka Umoja wa Mataifa na nchi zote kuhakikisha azimio hilo linatekelezwa.

Amewataka kutoa mashinikizo kwa utawala wa Israel ili kuzuia wizi wa maliasili za Palestina.

 4107227

Kishikizo: palestina hamas UNGA israel
captcha