IQNA

Bahman 22

Mamillioni ya Wairani washiriki katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

17:44 - February 11, 2023
Habari ID: 3476545
TEHRAN (IQNA)- Sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini zimefanyika kote nchini kwa ajili ya kuadhimisha miaka 44 ya mapinduzi hayo hayo, huku miji na vijiji vyote vya Iran vikishuhudia maandamano makubwa kuelekea viwanja na maeneo ya umma.

Leo Jumamosi tarehe 11 Februari imesadifiana na kutimia miaka 44 tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA.

Kuanzia jana usiku sauti za Takbira na nara za "Mauti kwa Marekani na Israel" zilisikika juu ya paa za nyumba na misikiti kote nchini huku vyombo vya moto kama treni, magari na meli vikipiga honi, ikiwa ni ishara ya maadhimisho yakubwa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiiislamu yanayofikia kileleni hii leo. 

Tarehe 22 Bahman (11 Februari) miaka 44 iliyopita Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu- walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya kusimika utawala wa Kiislamu.  

Kwa mnasaba wa kukumbuka ushindi huo adhimu, Mamilioni ya Wairani wameshiriki katika sherehe hizo ambapo wamesitiza mshikamano wao mkubwa, kizazi baada ya kizazi, na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, wakipeperusha bendera ya Uislamu na kuzidisha matumaini ya kupata ushindi watu wote wanaokandamizwa na kudhulumiwa duniani.

Sherehe za mwaka huu za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zina ladha ya kipekee, hasa baada ya kufeli njama kubwa iliyoanzishwa na madola ya kigeni dhidi ya Iran ya Kiislamu katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, iliyolenga usalama wa ndani na umoja na mshikamano wa taifa kwa kuibua ghasia na kuziunga mkono kupitia vita mseto vya kisiasa, kiuchumi na hujuma ya vyombo vya habari vya Magharibi. Hata hivyo hujuma na vita hivyo vilishindwa kutokana na mwamko, umakini, kusimama kidete, umoja na mshikamano wa wananchi na hekima ya viongozi wao.

Ushiriki mkubwa wa mamilioni ya wananchi wa Iran katika maandamano na sherehe za leo za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unatoa pigo kubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma kwa mabeberu wa kimataifa, ambayo bado hawajafahamu hali halisi ya Iran ya Kiislamu tangu baada ya Mapinduzi hayo hadi hizi sasa.

4121238

captcha