IQNA

Maoni

Siku ya Ghuba ya Uajemi nchini Iran

14:04 - May 01, 2023
Habari ID: 3476942
TEHRAN (IQNA)- Jana, tarehe 10 Ordibehest, 1402 Hijria Shamsia sawa na Aprili 30, ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kufukuzwa wakoloni wa Kireno katika maji ya Kusini mwa Iran hapo mwaka 1622, na inatambuliwa nchini Iran kuwa Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Ghuba ya Uajemi ni eneo la maji lenye zaidi ya kilomita za mraba 237,000 kando ya Bahari ya Oman na iko kati ya Iran na Rasi ya Arabia. Ghuba hii ni njia kuu ya baharini na ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Hudson Bay. Vilevile  inatambuliwa kuwa eneo muhimu na la kimkakati kimataifa kutokana na uwepo wa rasilimali kubwa za mafuta na gesi.

Jina la kihistoria la Ghuba hii limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kuwa ni Ghuba ya Uajemi au Bahari ya Uajemi; lakini katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zimetaka kupotosha jina hilo kutokana na uchechezi wa ukoloni wa nchi za Magharibi. 

Jina asili ni Ghuba ya Uajemi

Pamoja na hayo, Ghuba ya Uajemi ndilo jina asili ambalo limelosajiliwa kwenye vyanzo vya kale zaidi vya historia. Wanajiografia na wanahistoria wa Kiislamu kama vile Tabari, Masoudi na Yaqoubi wamesema kwa kauli moja katika maandishi yao kwamba, maeneo yote ya Ghuba ya Uajemi yalikuwa ya Iran katika nyakati za kabla ya kudhihiri Uislamu. Wagiriki wa kale pia waliita ghuba hiyo "Persikos Kolpos", yaani Ghuba ya Uajemi.

Kwa mujibu wa maagizo ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa mnamo Mei 14, 1999, jina la njia ya majini ambayo iko kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Peninsula ya Arabia ni "Ghuba ya Uajemi", na ni lazima kutumia jina kamili la "Ghuba ya Uajemi" katika nyaraka na machapisho ya Umoja wa Mataifa.

Ustaarabu uliokita mizizi

Uchimbaji wa kiakiolojia uliofanyika katika miji ya pwani ya Ghuba ya Uajemi umeonyesha utamaduni, sanaa na uchumi wa Wairani katika miaka mingi iliyopita. Ustaarabu huu umekita mizizi Kaskazini na Kusini mwa Ghuba ya Uajemi, na wakazi wa sasa wa sehemu zote na mwambao wa Ghuba ya Uajemi ni warithi wa utamaduni na ustaarabu wa Irani.

Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeitaja tarehe 10 Ordibehesht, siku ya kufukuzwa Wareno kwenye Lango Bahari la Hormuz, kuwa ni Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi. 

Uwanja wa ushindani

Kutokana na thamani zake za kijiografia na kiustaarabu, Ghuba ya Uajemi daima imekuwa uwanja wa ushindani na mivutano kati ya madola ya kikoloni na wavamizi. Miongoni mwa nyakati za kuwepo kwa maajnabi katika Ghuba ya Uajemi ni kipindi cha udhibiti wa miaka 150 wa Wareno katika njia hiyo ya majini na Lango-Bahari la Hormuz, ambao ulimalizika mwaka 1622.

Mnamo 1506 Wareno waliingia eneo la Ghuba ya Uajemi chini ya uongozi wa Kapteni Afonso de Albuquerque - baharia maarufu wa Kireno. Albuquerque aliamini kwamba nchi yoyote inaweza kutawala biashara ya dunia ikiwa itamiliki nukta tatu za Malaga, Aden na Hormuz.

Wazo hili liliwafanya Wareno wavamie na kukalia kwa mabavu visiwa vya Qeshm, Hormuz na Gambrun (kwa sasa Bandar Abbas) Kusini mwa Iran. Aprili mwaka 1622 jeshi la Iran lililokuwa likiongozwa na Imam Qoli-Khan lilikomboa Hormuz na kukiondoa kisiwa hicho kwenye makucha ya dola kubwa zaidi la kipindi hicho.

Wakoloni walikuwa na tamaa na Ghuba ya Uajemi

Wakoloni wa Kiingereza pia walikuwa na tamaa na Ghuba ya Uajemi lakini hatimaye walilazimika kuondoka katika eneo hilo. Waingereza walilishambulia eneo la Bushehr huko Kusini mwa Iran mara nne, na mara zote wanazuoni wa Kiislamu walitoa fatwa ya kukabiliana na wakoloni hao ambapo mashujaa kama Rais-Ali Delvari na Ahmadkhan Tangestani walipambana na mkoloni huyo mkongwe na kumshinda.

Ni wazi kuwa nafasi makshusi ya Ghuba ya Uajemi, ambayo ni kituo kikuu cha mawasiliano baina ya mabara matatu ya dunia, na kuwepo rasilimali za utajiri wa mafuta na gesi vinalifanya eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo muhimu na ya kistratijia duniani.

Lango Bahari la Hormuz

Njia hii ya majini ina umuhumu mkubwa kwa Iran. Karibu mafuta yote ya petroli ya Iran yanasafirishwa nje ya nchi kupitia Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz. Vilevile karibu asilimia 80 ya biashara ya Iran inafanyika kwa kusafirishwa kupitia maji ya Ghuba ya Uajemi. Zaidi ni kwamba, katika upande wa masuala ya kijeshi na kiusalama pia, Ghuba ya Uajemi ina nafasi makhsusi katika mahusiano ya kigeni ya Iran.

Kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza sera ya ujirani mwema na kueleza kwamba, njia hiyo muhimu ya baharini ni eneo salama na amani na nembo ya urafiki na kuishi pamoja kwa amani baina ya mataifa ya kanda hiyo, na kwamba madola ajinabi yanapaswa kuelewa kuwa usalama na amani ya eneo hilo itadhaminiwa na nchi za Ghuba ya Uajemi zenyewe.       

4137406

captcha