IQNA

Sura ya Qur'ani Tukufu /1

Tofauti kati ya ‘Rahman’ na ‘Rahim’ katika Qur'ani Tukufu

19:11 - September 25, 2023
Habari ID: 3477649
TEHRAN (IQNA) – Surah Al-Fatiha, ambayo ni sura ya kwanza ya Qur’ani Tukufu, imetajwa kuwa “Mama wa Qur'ani”.

Vile vile imeelezwa kuwa ni sura ya hadhi ya juu kabisa na tukufu zaidi ya Qur'ani Tukufu, kama Mwenyezi Mungu anavyosema katika aya ya 87 ya Sura Hijr kwamba: ” Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu.”. Pia, ni Sura pekee ambayo lazima isomwe katika sala ya kila siku.

Sura Al-Fatiha imeanza kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu, Rahman (Mwingi wa rehema) na Rahim (Mwenye kurehemu).

“Sifa njema zote ni za Mwenyeezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote;  Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu;.” (Aya ya 2-3)

Mwenyezi Mungu amejitambulisha mara kwa mara kwa sifa hizi mbili: Rahman na Rahim.

Wafasiri wamesema kuhusu tofauti kati ya maneno hayo mawili kwamba Rahman inarejea kwenye upana na ujumuishi wa huruma ya Mwenyezi Mungu ambayo inawanufaisha watu wote, wawe ni waumini au makafiri, ambapo Rahim anaelezea rehema ya milele na baraka ya milele ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kwa ajili tu ya waaminifu. (Tafsiri ya  Qur'ani ya Al-Mizan)

Vile vile imepokewa kutoka kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kwamba “Mwenyezi Mungu ana Rahma (huruma) 100, moja kati ya hizo Ameiteremsha duniani na kuwagawanya waja Wake. Ni kwa Rahma hUyo mmoja ndipo watu wanakuwa wema na wanaonyeshana ihsani. Ama kuhusu Rahma 99 nyingine, Mwenyezi Mungu atawarehemu waja wake Siku ya Kiyama”. (Majma al-Bayan)

Ikumbukwe kwamba nambari 100 hapa ni kwa ajili ya kuonyesha tu wingi wa rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu rehema zake hazina kikomo na hazipimiki.

Surah Al-Fatiha pia inazungumzia Sirat al-Mustaqim (Njia Iliyo Nyooka). Sirat al-Mustaqim maana yake ni njia iliyo wazi na pana na laini isiyogeukia upande wowote. Katika Qur'ani Tukufu, Sirat al-Mustaqim ina maana ya njia ya kumwabudu Mwenyezi Mungu, imani ya kweli na kujitolea kwa amri za Mungu. Kama tunavyosoma Aya ya 7 ya Surah Al-Fatiha isemayo " Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea" , tunasoma katika Aya ya 161 ya Surah Al-An’am, “Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa,…"

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 59 ya Sura An-Nisa kwamba njia hii ilihitaji utiifu katika hali tatu: “Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.”

3478334

captcha