IQNA

Watetezi wa Palestina

Rabi: Wazayuni ‘Wanatumia Vibaya’ Uyahudi kuendeleza uvamizi haramu ardhi za Palestina

7:06 - December 12, 2023
Habari ID: 3478024
IQNA – Rabi au Kuhani wa Kiyahudi mwenye makazi yake nchini Marekani anasema utawala haramu wa wa Israel unatumia vibaya dini ya Kiyahudi ili kuendeleza ukatili na uvamizi wake katika ardhi za Wapalestina.

Utawala huo umekuwa ukishambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba, baada ya makundi ya mapambano ya Kiisalmu au muqawama huko Palestina kuanzisha operesheni ya kushtukiza katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ili kukabiliana na ongezeko la ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Katika vita hivyo vya mauaji ya halaiki, Israel kwa himaya ya Marekani  imewaua Wapalestina wasiopungua 18,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, huku wengi wa wakaazi milioni 2.3 wa Gaza wakilazimika kuyahama makazi yao.

Mauaji hayo ya halaiki ya Israel dhidi ya Palestina yampingwa na watu kote ulimwenguni wanaotaka kusitishwa kwa mapigano mara moja.  Umoja wa Mataifa umeshindwa kuulazimu utawala katili wa Israel usitishe jinai dhidi ya Wapalestina. Kuna idadi kubwa ya Mayahudi duniani ambao pia wanaulaani utawala haramu wa Israel kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina.

"Tumelazimika kupaza sauti zetu kwa uwazi na kupinga ukatili wa Kizayuni kwa sababu Wazayuni wanaendelea kutumia vibaya jina la Wayahudi na dini ya Kiyahudi," Kuhani Dovid Feldman, msemaji wa Neturei Karta International, aliiambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) katika mahojiano. .

"Kuwepo kwa taifa la Israeli, uvamizi unaoendelea, ikiwa ni pamoja na ukatili wote tangu kuanzishwa Israel mwaka 1948, ni ukiukaji wa Uyahudi na ni uhalifu na wa kinyama," alisema.

Akinukuu imani za Kiyahudi, Feldman alisema "Wayahudi wamekatazwa kuunda taifa lo wenyewe" kwa kuwa Mwenyezi Mungu "aliwaweka uhamishoni", akisisitiza kwamba wamepigwa marufuku kukomesha amri hii ya kimungu.

"Nukta hii hasa ni muhimu kwa sababu utawala wa Israel unatekeleza mauaji na unakali ardhi kwa mabavu, ambayo yote ni marufuku kabisa katika dini ya Kiyahudi," alisema, akiongeza kuwa Wayahudi wanatakiwa kuishi kama raia waaminifu na majirani wenye amani katika nchi wanazoishi.

Hata hivyo, alisisitiza, “Harakati ya Kizayuni inatumia dini ya Kiyahudi kuhalalisha ukaliaji wao na kuhalalisha jinai zao dhidi ya ubinadamu. Dini ya Kiyahudi inakataza kuua na kuiba, Inasikitisha kwamba yote haya yanatokea, kwa madai kuwa ni kwa mujibu wa mafundisho ya Torati. Huu  ni uwongo na ni  kinyume kabisa cha Torati na Uyahudi."

Akisisitiza kwamba Palestina ni ya wakazi wake wa asili wa ardhi yao, Feldman alisema "Palestina ilikuwa makazi ya watu wa dini tofauti, na hata waliowachache walikuwa wakiishi kwa amani ... watu wa imani ya Kiyahudi na Kikristo ni wachache na Waislamu ndio walio wengi." Alibainisha kuwa amani hii ilivurugika wakati Wazayuni walipoanzisha mradi wao wa kikoloni.

Alikuwa akirejelea Azimio lenye utata la 1917 la Balfour, lililobuniwa na madola ya Magharibi, ambapo ahadi ya nchi ya Palestina kwa Wayahudi ilitolewa bila kushauriana na wakazi wa kiasili. Tamko hilo likizingatiwa kuwa ni la kikoloni, lilipuuza haki na matakwa ya Wapalestina asilia waliopinga uvamizi wa Wazayuni na kukaliwa kwa mabavu ardhi yao.

Mnamo 1948, vikosi vya kijeshi vya Kizayuni vilitekeleza kampeni ya kikatili ya maagamizi ya kikaumu maarufu kama Nakba au janga. Jinai hiyo ilijumuisha uharibifu wa maeneo ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na vijiji na miji zaidi ya 500, na kusababisha vifo vya takriban Wapalestina 15,000. Zaidi ya hayo, karibu Wapalestina 750,000 walifukuzwa kwa nguvu kutoka kwa nyumba zao.

"Lazima tukubali kwamba ni uvamizi wa kikatili wa Palestina ambao umeharibu amani na hadi leo hii unasababisha mzunguko wa umwagaji damu unaoendelea," Feldman alisisitiza, akiashiria sababu kuu ya vita katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

"Sisi Wayahudi tunapaswa kuonyesha shukrani kwa watu ambao wametufanyia mema tu," alisema, akiongeza kuwa Wayahudi "waliuawa na kuteswa" katika baadhi ya nchi katika miaka 2000 iliyopita, hata hivyo, ni mataifa ya Kiislamu na Kiarabu ambayo yaliwakaribisha Wayahudi katika nyumba zao.

"Ni jambo la kuchukiza na ni kinyume cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu, badala ya kuonyesha shukrani kwa watu wa Palestina, wameira ardhi yao, na kisha kuwashutumu watu wa Palestina kuwa ni waovu na wanataka kuwaua Wayahudi. Haya yote ni ya kuchukiza, na si kweli,” alisema.

Nchi za Magharibi zinaendelea kuunga mkono uvamizi huo huku vyombo vyao vikuu vya habari vikizingatia propaganda za Israel kuhusu mzozo huo bila kutaja sababu kuu ya mzozo wa Palestina.

Hata hivyo, Feldman, anasisitiza kwamba Wazayuni hawana tena udhibiti kamili juu ya taarifa kuhusu Palestina.

Utawala "Daima walijaribu kuwaharibia jinai watu wa Palestina, ili kupotosha fikra za walimwengu kuhusu jinai zao kwa kudai Waislamu si wastahamilivu," Feldman alisema.

"Yote haya ni kuhalalisha jinai yao ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina," alisisitiza, na kuongeza, "maoni ya umma yanabadilika kadri watu wanavyojifunza zaidi kuhusu dhuluma za miongo kadhaa dhidi ya Wapalestina."

captcha