IQNA

Iran yatahadharisha kuhusu njama za maadui baada ya hujuma msikitini Afghanistan

7:46 - October 16, 2021
Habari ID: 3474428
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali kitendo cha magaidi wakufurishaji kuushambulia msikiti wa Bibi Fatima wakati wa Sala ya Ijumaa mjini Kandahar nchini Afghanistan.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesima hujuma dhidi ya msikiti huo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni jinai dhidi ya binadamu ambayo imetekelezwa na magaidi wakufurishaji. Taarifa hiyo imesisitiza kuhusu umuhimu wa umoja wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni ili kukabiliana na njama za maadui. Halikadhalika taarifa hiyo imesisitiza kuhusu ulazima wa kujiepusha na utumiaji mabavu pamoja na misimamo mikali kwa jina la Uislamu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema  kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kulinda maeneo ya ibada ya nchini Afghanistan kufuatia tukio hilo la kusikitisha jana na pia hujuma ya wiki iliyopita huko Kunduz

Zaidi ya watu sitini waliuawa shahidi wakati milipuko mitatu ilipoulenga msikiti wa Bibi Fatima wakati wa Sala ya Ijumaa jana.

Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh kimedai kuhusika na hujuma hiyo. Wiki iliyopita pia kundi hilo hilo la magaidi wakufurishaji lilidai kuhusika na hujuma dhidi ya msikiti mwingine wa Mashia katika mji wa kunduz ambapo waumini wasipungua sitini pia waliuawa shahidi.  Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini hujuma hizo za kigaidi dhidi ya misikiti ya Mashia zinachochewa na Marekani ili kuivuruga serikali mpya ya Taliban nchini Afghanistan na pia kwa ajili ya kuwaangamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.

4005148

captcha