IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 52

Taswira ya Baraka za Mwenyezi Mungu na adhabu katika Sura At-Tur

19:20 - December 31, 2022
Habari ID: 3476334
TEHRAN (IQNA)- Mengi yamesemwa kuhusu akhera na maisha baada ya kifo na miongoni mwa imani kuu juu yake ni ile ya watu wa dini hasa Waislamu wanaoamini kuwa matendo ya kila mtu yatapimwa Siku ya Kiyama na kwa kuzingatia tathmini hiyo atakwenda ama peponi au motoni.

At-Tur ni Sura ya 52 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 49 na iko katika Juzuu ya 27. Ni Makki (iliteremshwa Makka) na ni sura ya 76 aliyoteremeshiwa  Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Katika aya ya kwanza, Mwenyezi Mungu anaapa kwa At-Tur (Mlima Sinai), na kwa hiyo Sura imepewa jina hilo.

Mlima Sinai ni mahali patakatifu palipo Palestina. Nabii Musa (AS) alizungumza na Mwenyezi Mungu na akapokea wahyi katika mlima huo. Jina la At-Tur limetajwa mara kumi katika Qur'ani Tukufu.

Kulingana na Tafsiri ya Al-Mizan ya Qur'ani Tukufu, mada kuu ya Sura At-Tur ni kuwaonya wale wanaoonyesha uadui kwa ukweli. Inawatahadharisha makafiri kuhusu adhabu ya Mwenyezi Mungu inayowangoja Siku ya Kiyama, ikisisitiza kuwa adhabu hiyo ni ya hakika.

Kisha Sura inafafanua baadhi ya vipengele vya adhabu na pia baadhi ya baraka wanazopewa wale wanaokwenda peponi, ambao  ni wale wanaofanya wema katika dunia hii na wana imani na Mwenyezi Mungu.

Maudhui ya Sura yanaweza kugawanywa katika sehemu sita:

Aya za mwanzo zinazoanza na baadhi ya viapo zinahusu suala la adhabu ya Mwenyezi Mungu, moto wa Jahanam na dalili za Siku ya Kiyama.

Sehemu nyingine inaangazia baraka za Mwenyezi Mungu zinazowangoja wachamungu peponi.

Pia inazungumzia utume wa Mtukufu Mtume Muhammad  (SAW) na inajibu kwa ufupi shutuma zilizotolewa dhidi yake na maadui.

Dhamira nyingine iliyosisitizwa katika sura hii ni upweke wa Mwenyezi Mungu na kuuthibitisha kwa hoja zilizo wazi na zenye mvuto.

Sura inarejea tena Siku ya Hukumu au Siku ya Kiyama na inaeleza baadhi ya vipengele vyake.

Katika aya za mwisho, Sura inatoa baadhi ya amri kwa Mtume Muhammad (SAW) kuhusu subira na uthabiti pamoja na kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia inaahidi msaada wa Mwenyezi Mungu kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

captcha