IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 53

Safari ya kwenda mbinguni na mazungumzo ya Mtume Muhammad SAW na Mwenyezi Mungu katika Surat An-Najm

21:19 - January 03, 2023
Habari ID: 3476353
TEHRAN (IQNA) – Moja ya imani za Waislamu ni kuhusu safari ya Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kwenda mbinguni. Katika safari hii ya usiku, inayojulikana kama Mi’raj (kupanda), Mtume Muhammad (SAW) alisafiri kwenda mbinguni na kuzungumza na baadhi ya malaika, mitume wengine na Mwenyezi Mungu.

An-Najm ni jina la sura ya 53 ya Qur'ani Tukufu, ambayo ina aya 62 na imo katika Juzuu ya 27. Ni Makki na ni sura ya 23 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Baadhi wanaamini kuwa ni Sura ya kwanza ambayo Mtume Muhammad (SAW) aliisoma hadharani kwenye Ka’aba tukufu baada ya kuwaalika wazi watu kuingia katika Uislamu.

Sura inaitwa An-Najm kwa sababu katika Aya ya kwanza, Mwenyezi Mungu anaapa kwa Najm (nyota) na wakati inaposhuka. Neno Najm katika maumbo yake ya umoja na wingi limetajwa mara 13 katika Qur'ani Tukufu.

Madhumuni ya jumla ya Surah An-Najm ni kuweka mkazo juu ya mada tatu: Uungu, Utume na Ufufuo. Pia inazungumzia ukweli wa wahyi, mawasiliano ya moja kwa moja ya Mtume Muhammad (SAW) na Malaika Jibril (Gabriel), kisa cha Mi’raj ya Mtukufu Mtume.

Sura hii inawashutumu makafiri kutokana na kuabudu masanamu na inazungumzia ukweli kwamba milango ya toba iko wazi na kwamba kila mtu anawajibika kwa matendo yake, pamoja na hatima ya mataifa yaliyotangulia ambayo yalisisitiza kuendeleza uadui dhidi ya ukweli.

Mwanzoni mwa Sura, Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba Mtume Muhammad (SAW) anapokea Wahyi moja kwa moja kutoka kwa Malaika Jibril na kwamba hasemi isipokuwa yale yaliyoteremshwa kwake.

Katika sehemu nyingine, Sura inazungumzia safari ya Mtume Muhammad (SAW) kwenda mbinguni na inaonyesha baadhi ya sehemu za safari hiyo.

Kisha inakosoa ushirikina wa makafiri kuhusu masanamu na masuala mengine ambayo yanatokana na matamanio na vishawishi na kuwakumbusha kuwa milango iko wazi kwa ajili ya kutubia. Inaangazia msamaha wa Mwenyezi Mungu na pia ukweli kwamba kila mtu anawajibika kwa matendo yake.

Kisha, Sura inazungumzia suala la kufufuliwa Siku ya Kiyama na kulithibitisha kwa sababu zilizo wazi na zenye mantiki. Pia inahusu hatima chungu ya watu waliotangulia ambao walikuwa na uadui kwa ukweli na kusisitiza juu ya uadui wao.

Mi’raj ya Mtume Muhammad (SAW) ni miongoni mwa masuala makubwa yaliyotajwa katika Sura hii. Usiku wa Mi’raj, Mtume (SAW) alisafiri kutoka Makka hadi Msikiti wa Al-Aqsa huko Palestina na kutoka hapo kwenda mbinguni. Kwa mujibu wa riwaya za vyanzo vya Kiislamu, katika safari hiyo, alizungumza na baadhi ya malaika pamoja na watu wa peponi na motoni. Mtume (SAW) pia alizungumza na baadhi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na pia kukawa na mazungumzo baina yake na Mwenyezi Mungu.

captcha