IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu / 56

Mwisho wa Matukio ya Ulimwengu Yamefafanuliwa katika Surah Al-Waqi’a

11:06 - January 15, 2023
Habari ID: 3476405
TEHRAN (IQNA) – Kuna maoni na nadharia tofauti kuhusu kitakachotokea mwishoni mwa wakati. Wengi wao wanatabiri kwamba matukio ya kustaajabisha na makali yatatokea duniani. Surah Al-Waqi’a ya Qur’ani Tukufu inaonyesha baadhi ya matukio hayo.

Al-Waqi’a ni sura ya 56 ya Qur’ani Tukufu ambayo ina aya 96 na iko katika Juzuu ya 27. Ni Makki na ni Sura ya 44 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Waqi’a ni neno linalomaanisha tukio au kutokea  na ni mojawapo ya majina ya Siku ya Hukumu au Siku ya Kiyama. Jina la Surah linatokana na neno Waqi’a katika aya ya kwanza.

Surah Al-Waqi’a inazungumza kuhusu Siku ya Kiyama na matukio yake. Ni siku ambayo watu watafufuliwa na yale wanayoyafanya katika ulimwengu huu yatatathminiwa.

Sura inaeleza kwanza baadhi ya matukio ya siku hiyo, ikiwa ni pamoja na kutikisika kwa ardhi kwa nguvu, kutokea matetemeko ya ardhi na kuporomoka kwa milima. Kisha inawagawanya watu siku hiyo katika makundi matatu na kueleza hatima yao: 1- Waliotangulia, 2- Watu wa Kulia, na 3- Watu wa Kushoto.

Kisha Sura inataja sababu za kuwajibu watu wa kushoto wanaomkanusha Mwenyezi Mungu, Qur’ani  na Siku ya Kiyama, na kuwalingania watu kwenye Tauhidi na kuamini Siku ya Kiyama.

Mada zilizotajwa katika Sura ni pamoja na: Kuanza kwa Siku ya Kiyama kwa matukio makali na ya kutisha, watu kugawanywa katika makundi matatu siku hiyo kwa kuzingatia matendo yao hapa duniani, hadhi ya watu walio karibu na Mwenyezi Mungu na  malipo ya peponi, kundi la pili, yaani Watu wa Kulia na baraka za Mwenyezi Mungu zilizo juu yao  na kundi la tatu, Watu wa Kushoto, na adhabu chungu watakazozipata motoni.

Pia kuna sababu zilizotajwa kuthibitisha kuwepo Siku ya Kiyama ikiwa ni pamoja na kufafanua juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, uumbaji wa watu kutoka kwa manii, kuwepo kwa maisha katika mimea, mvua, na mwanga wa moto, ambazo ni ishara za Mwenyezi Mungu.

Sura hiyo pia inaonesha jinsi watu wanavyokufa na kuhama kutoka katika dunia hii hadi nyingine na inazungumzia malipo ya waumini na adhabu kwa makafiri huko akhera.

Kwa mujibu wa Surah Al-Waqi’a, Watu wa Kulia ni wale wanaokwenda peponi na Watu wa Kushoto ni wale wanaoingia motoni.

Ama walio shinda, aya ya 10 ya Sura inasema: “ Waliotangulia ndio waliotangulia.”.

Wafasiri wa Quran wana mitazamo tofauti kuhusu aya hii. Kwa kuzingatia aya nyinginezo za Qur'an Allamah Seyed Mohammad Hossein Tabatabai anaamini kwamba katika Aya ya 10 ya Surah Al-Waqi'a,  “Waliotangulia ndio waliotangulia.”  inaashiria walio mbele zaidi (katika imani na wema) na pia inawahusu walio mbele zaidi katika kupokea malipo yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

captcha