IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 62

Ufafanuzi wa Qur'ani kuhusu wale wasiojali Sharia za Mwenyezi Mungu

20:25 - February 21, 2023
Habari ID: 3476597
TEHRAN (IQNA) - Katika hadithi za manabii wa kiungu tunasoma kuhusu makundi ya watu wanaojiona kuwa wafuasi wa Mitume wa Mwenyezi Mungu lakini kwa hakika hawajali amri za Mwenyezi Mungu na mafundisho ya manabii.

Qur'an Tukufu, katika Sura Al-Jumuah, inawaelezea watu kama hao kuwa ni madhalimu na kuwafananisha na mnyama aliyebeba mizigo.

Al-Jumuah ni Sura ya 62 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 11 na iko katika Juzuu ya 28. Ni Madani na ni sura ya 109 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Katika Uislamu, Jumaah (Ijumaa) ni siku ya mwisho ya juma. Sura inazungumzia kanuni na taratibu za sala ya Ijumaa na kwa hivyo jina lake linatokana na maudhui hiyo. Mwenyezi Mungu katika sura hii anasisitiza umuhimu wa Sala ya Ijumaa na anawaamrisha Waislamu kuepukana na biashara wakati wa Sala ya Ijumaa.

Sura ina dhamira kuu mbili: Ya kwanza Tauhidi yaani kumpwekesha Mwenyezi Mungu, hadhi ya utume na suala la siku ya kiyama na pili umuhimu na vipengele vya Sala ya Ijumaa.

Inaanza kwa kurejelea ukweli kwamba viumbe vyote duniani na mbinguni vinamtukuza Mungu. Vile vile inasema kwamba Mwenyezi Mungu amemteua miongoni mwa wasiojua kusoma (Waarabu) mtume kutoka kwa nafsi zao ili awaongoze.

Sura inawaonya Waislamu wasiwe kama Mayahudi walioishi zama za Mtukufu Mtume Muhammad (SAW). Inasema walibeba Taurati pamoja nao lakini hawakuifanyia kazi, ikithibitisha kwamba walikuwa na imani ya dhahiri tu katika kitabu hicho na hawakuwa na ufahamu wa kweli wa mafundisho yake. Inawafananisha walio hivyo na punda. “Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anaye beba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu walio kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.” (Aya ya 5)

Sura inawataka Waislamu kushiriki katika Sala ya Ijumaa, ibada ambayo inakuza umoja wa Kiislamu na kusaidia kuimarisha mafungamano kati ya watu na uongozi. Ndio maana Qur'ani Tukufu inasema kuhudhuria Sala ya Ijumaa kuna thawabu sio tu huko akhera bali hata duniani.

Miongoni mwa maagizo muhimu sana katika Sura hii ni kuacha biashara unapofika wakati wa swala ya Ijumaa. “ Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua.. (Aya ya 9)

Sura inawakosoa wale wanaoacha sala kwenda kununua na kuuza vitu, ikisema hawana ufahamu mzuri wa kanuni za Mwenyezi Mungu. “Na wanapo iona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.” (Kifungu cha 11)

captcha